May 23, 2022 09:43 UTC
  • UNHCR: Kuna wakimbizi zaidi ya 100 kote ulimwenguni

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, kuna zaidi ya watu milioni 100 ambao ni wakimbizi katika maeneo mbalimbali ya dunia.

Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la UNHCR inaeleza kuwa, kwa mujibu wa nyaraka mpya watu ambao wanakimbia machafuko, mapigano, mateso na vitendo vya ukiukaji wa haki za biinadamu katika maeneo yao wameongezeka na hivi sasa kuna zaidi ya watu milioni 100 kote ulimwenguni ambao ni wakimbizi.

Ripoti ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) iliyotolewa leo Jumatatu imeashiria vita vya Ukraine na machafuko na mapigano ya muda mrefu katika baadhi ya mataifa kama ya Ethiopia, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kueleza kwamba, machafuko hayo ni chimbuko la kuongezeka idadi ya wakimbizi duniani.

Mataifa mengine ambayo raia wake wamelazimika kuyakimbia makazi yao ni Myanmar, Afghanistan, Syria, Libya na Iraq.

Wakimbizi wa Ukraine

 

Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) yametangaza kuwa, raia milioni 14 na laki nne wa Ukraine wamelazimika kuwa wakimbizi tangu vita vilipoanza mwezi Februari mwaka huu. 

Ripoti ya UNHCR inaonyesha kuwa, Syria inaongoza kwa kuwa na raia wengi wasio na makazi ambapo kuna wakimbzi milioni 6,700,000, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo 5,300,000, Colombia 5,200,000 huku Afghanistan na Yemen zikiwa na raia 4,300,000 kila moja ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Tags