May 24, 2022 07:19 UTC
  • IMF: Hali ya uchumi wa dunia ni mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu Vita vya Pili vya Dunia

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Kimataifa wa Fedha IMF ametoa indhari kuhusiana na kuongezeka mfumuko wa bei na kuzorota uchumi duniani kote.

Kristalina Georgieva ametoa indhari hiyo katika hotuba ya hafla ya ufunguzi wa mkutano wa Jukwaa la Dunia la Uchumi unaofanyika mjini Davos, Uswisi.

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa IMF ameeleza kuwa, kutokana na janga la dunia nzima la virusi vya corona, vita vya Ukraine na mabadiliko ya tabianchi, nchi za ulimwengu zimekumbwa na ughali wa bidhaa na uzorotaji wa uchumi ambao haujawahi kushuhudiwa.

Georgieva ameongeza kuwa, "tangu wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia hadi sasa, uchumi wa dunia uko kwenye hali mbaya zaidi na unakabiliwa na mazingira magumu."

Mkuu huyo wa IMF ameeleza kuwa, athari za kupanda kwa bei za bidhaa za chakula na nishati ni kubwa mno kwa familia na akaongezea kwa kusema: "hali hii mbaya imesababisha matatizo mengi kwa nchi za ulimwengu wa tatu, hivyo zinahitaji kusaidiwa."

Bi Kristalina Georgieva amezitaka nchi tajiri zipunguze vizuizi vya kibiashara na kuboresha mifumo ya kifedha ya nje ya mipaka yao ili kuzisaidia nchi dhaifu nazo zikue na kustawi kiuchumi.

 Marekani na nchi nyingine za Ulaya zinakabiliwa na ongezeko la mfumuko wa bei katika uchumi na kuongezeka kwa gharama za maisha.../

Tags