May 24, 2022 11:24 UTC
  • Baraza Kuu la UN latoa wito wa kuungwa mkono haraka nchi zilizoathiriwa na mzozo wa chakula

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepatisha azimio linaloitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono na kusaidiwa haraka nchi zilizoathiriwa na mzozo wa usalama wa chakula kupitia hatua za pamoja, huku maonyo kuhusu bei ya chakula duniani yakiongezeka.

Tahadhari ya uhaba wa chakula duniani imefikia kiwango cha juu zaidi kutokana na vita vya Ukraine na Russia, na upatikanaji wa chakula umekuwa mgumu zaidi kwa watu wengi duniani.

Jumatatu Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio kuhusu "Hali ya Uhaba wa Chakula Duniani", ambalo limeunga mkono mpango wa Katibu Mkuu wa kuunda kikundi cha kukabiliana na mgogoro wa kimataifa kuhusu masuala ya chakula, nishati na kifedha.

Azimio hilo limezitaka nchi wanachama na wadau wengine kudumisha kilimo na usambazaji wa chakula sambamba na kusisitiza haja ya kudumisha njia za biashara na kufungua masoko ya mtiririko wa chakula, mafuta, mbolea za kemikali na mazao mengine ya kilimo.

Sehemu nyingine za azimio hilo zinatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na makundi ya madola makubwa ya G7 na G20, kuweka usalama wa chakula mbele ya ajenda zao na kuunga mkono juhudi za pande kadhaa za kutafuta ufumbuzi wenye gharama nafuu wa mgogoro uliopo hivi sasa.

Watoto wanaokumbwa na njaa nchini Afghanistan

Azimio hilo pia linazitaka nchi wanachama na washikadau kujiepusha na kujirundikia chakula na bidhaa.

Mkuu wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) David Beazley hivi karibuni alisema kushindwa kufunguliwa tena bandari nchini Ukraine kutakuwa sawa na tangazo la vita dhidi ya usalama wa chakula duniani, na kusababisha kukosekana kwa utulivu katika nchi za dunia kutokana na njaa sambamba na kupelekea kuongezeka uhamiaji.

Wizara ya mambo ya nje ya Russia imekanusha madai ya kufunga bandari za Ukraine na kuyataja kuwa yasiyo na msingi.

Vikwazo vya madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani dhidi ya Russia vimelazimisha makampuni ya kimataifa kukata uhusiano wa muda mrefu wa kibiashara na kuondoka Russia na hali hii imevuruga usambazaji bidhaa muhimu za chakula na kilimo.