May 25, 2022 02:16 UTC
  • Uhaba wa chakula duniani na matokeo yake

Linda Thomas Greenfield, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa, indhari ya uhaba wa chakula duniani inayotokana na vita vya Ukraine na Rusia imefikia katika kiwango cha juu kabisa na mazingira ya akthari ya watu ulimwenguni ya kupata chakula yamezidi kuwa magumu siku baada ya siku.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, katika kulinganisha kuanzia moja mpaka kumi, indhari ya uhaba wa chakula duniani kuna uwezekano ikawa imefikia namba kumi, kwani mgogoro wa vita hadi sasa umezidi kuhatarisha suala la usalama wa chakula.

Suala la kudhamini chakula hususan katika miongo ya hivi karibunin limekuwa gumu zaidi na hili limesababishwa na mambo tofauti kama mabadiliko ya tabianchi na msambao wa virusi vya Corona ulimwenguni. Filihali, kudhamini chakula imekuwa daghadagha na wasiwasi mkubwa kwa walimwengu ingawa vita vya Russia na Ukraine vimechochea zaidi hali hii.

Kanali ya Televisheni ya CNN imeripoti kuwa, watu milioni 811 hupanda kitandani usiku kwa ajili ya kulala hali ya kuwa wana njaa huku watu milioni 44 katika nchi 38 duniani wakikabiliwa na njaa kali. Hii ni katika hali ambayo, Mpango wa Chakula Duniani (WFP) unakadiria kwamba, katika kipindi cha kuanza vita vya Ukraine hadi sasa bei ya ngano na mahindi kimataifa imeongezeka baina ya asilimia 18 na 30.

Hali hii imepelekea kuongezeka uhaba wa chakula na kuongezeka bei ya bidhaa za chakula kimataifa hususan katika nchi dhaifu katika bara la Afrika. Kwa mujibu wa takwinu ni kuwa, takriban watu milioni 346 barani Afrika wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula.

Eneo la Pembe ya Afrika ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na baa la njaa

 

Russia na Ukraine kwa utaratibu ni wauzaji wakubwa wa ngano duniani. Vita vya Ukraine vimelifanya suala la usafiri na uchukuzi wa ngano kupitia Bahari Nyekundu likabiliwe na mushkeli. Hii ni katika hali ambayo, akthari ya ardhi za kilimo haikuwezekana kupanda mazao kutokana na ukosefu wa usalama na watu kuyakimbia makazi yao. Bandari zinazotumika kusafirisha makontena kwa makontena ya bidhaa za chakula hasa ngano zimefungwa kutokana na vita na hakuna uwezekano wowote wa kusafirisha mizigo na hata bidhaa za chakula zilizokuwa tayari kwa ajili ya kusafirishwa zimekwama katika bandari hizo.

Katika mazingira kama haya viongozi wa Marekani wanafanya njama na hila za kuionyesha Russia kuwa ndio msababishaji wa uhaba huu wa chakula duniani. Hii ni katika hali ambayo, uingiliaj wa Marekani na mvutano wa kisiasa wa Washington na Moscow ndio mambo yaliyochochea kuni za moto wa vita baina ya Russia na Ukraine.

Kadhalika hatua ya pupa ya viongozi wa Marekani ya kuiwekea vikwazo vizito Russia na kuyachochea mataifa ya Ulaya ni njama ya wazi ya kuitenga Russa. Ukweli wa mambo ni kuwa, viongozi wa Marekani walichofanya katika kuishinikiza Russia ni kutanguliza mbele maslahi yao ya kisiasa.

Anatoly Antonov, balozi wa Russia nchini Marekani anasema: Mgogoro wa chakula duniani umeshadidi baada ya wimbi la vikwazo vya upande mmoja na visivyo vya kisheria dhidi ya Russia.

Msaada wa chakula Sudan Kusini

 

Timu ya kimataifa ya wataalamu imetahadharuisha kuhusiana na suala la chakula kwa kusema: Vita vya Ukraine ni kimbunga kwa ajili ya mgogoro mpya na mkubwa wa chakula, mgogoro ambao inawezekana kuuepuka.

Pamoja na hayo, viongozi wa Marekani na Ulaya ambao nchi zao zenyewe hivi sasa zinakabiliwa na matatizo ya nishati ya mafuta na uhaba wa bidhaa za chakula, wanafanya njama za kuionyesha Rusia kwamba, ndio msababishaji wa hali ya sasa inayokabiliwa nayo dunia.

Anatoly Antonov, balozi wa Russia nchini Marekani ameyataja matamshi ya viongozi wa Magharibi waliodai kwamba, eti vikwazo vyao havijumuishi bidhaa za chakula na watoto kuwa ni hadaa ni upotoshaji mkubwa. Anasema, katika uga wa fedha pamoja na usafiri na uchukuzi, vikwazo hivyo vimekuwa na taathira hasi na tena ya moja kwa moja kwa soko la dunia la chakula.

Vyovyote itakavyokuwa, hivi sasa sauti ya kengele ya hatari ulimwenguni inasikika na inaonekana kuwa, kuendelea hali hii, kutaifanya dunia ikabiliwe na hali mbaya ya uhaba mkubwa wa chakula ambapo natija ya hilo ni kuwa wahanga wa maelfu ya watu duniani ambao watapoteza maisha kutokana na baa la njaa.

Tags