May 25, 2022 03:33 UTC
  • Jinai mpya Marekani, watoto wadogo 19 wauliwa kwa umati na gaidi shuleni

Televisheni ya CNN ya Marekani imeripoti kuwa watoto wadogo wasiopungua 19 wameuawa kwa umati baada ya gaidi mmoja aliyetajwa kwa jina la Salvador Ramos kuvamia shule yao huko Uvalde Texas jana Jumanne kwa wakati wa eneo hilo.

Gavana wa jimbo la Texas amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, mtuhumiwa wa mauaji hayo ambaye naye ameuawa kwa kupigwa risasi alikuwa ni kijana wa miaka 18 na alikuwa anasoma skuli hiyo ya sekondari huko Uvalde. 

Baadhi ya vyombo vya habari ikiwemo televisheni ya ABC News vimeitaja idadi ya watoto wadogo waliouliwa kwa umati na gaidi huyo ni 18 lakini mapema leo asubuhi televisheni ya CNN pia ya huko huko Marekani imesema idadi ya watoto wadogo waliuliwa kwa umati ni 19 na watu wazima waliouwa ni wawili akiwemo mwalimu wa kike wa darasa lililovamiwa na gaidi huyo.

Mauaji ya kiholela ni jambo la kawaida sana nchini Marekani

 

Gaidi huyo alisambaza picha za silaha kwenye ukurasa wake wa Instagram kabla ya kufanya jinai hiyo ya kutisha. Taarifa zaidi zinasema kuwa, Ramos alimpiga risasi kwanza bibi yake nyumbani kabla ya kwenda kwenye skuli hiyo ya sekondari ya Uvalde huko Texas na kuwaua kwa umati watoto wadogo wa darasa la nne waliokuwa wanasoma darasani pamoja na mwalimu wao.  Bibi wa gaidi huyo yuko mahututi hospitalini hivi sasa.

Mauaji ya umati na ya kiholela ni jambo la kawaida sana nchini Marekani. Televisheni ya CNN imetangaza kuwa, mwaka 2020 jimbo la Mississippi ambalo sheria za kubeba silaha moto ni nyepesi mno, ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya watu waliouawa kwa silaha hizo.