May 25, 2022 07:24 UTC
  • Mfumuko wa bei za vyakula, mgogoro wa pili kwa ukubwa UK; vikwazo vya Russia vyachangia

Matokeo ya uchunguzi wa maoni waliofanyiwa wananchi wa Uingereza yanaonesha kuwa, mfumuko wa bei za vyakula umefikia kiwango cha juu kabisa nchini humo kuliko miaka 13 iliyopita na kwamba mfumuko huo ni mgogoro wa pili kwa ukubwa huko Uingereza baada ya kupanda vibaya bei ya nishati.

Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi ya kimataifa ya Kantar Worldpanel ya Uingereza yanaonesha kuwa, bei za vyakula zimepaa kwa asilimia 7 kutoka asilimia 5.9 zilivyokuwa mwezi uliopita wa Aprili.

Ripoti ya karibuni kabisa ya taasisi ya kimataifa ya kukusanya maoni iitwayo Kantar Worldpanel inaonesha kuwa, bidhaa za chakula nchini Uingereza katika wiki ya 12 inayomalizikia tarehe 15 Mei mauzo ya maduka makubwa nchini humo yamepungua kwa asilimia 4.4 ikilinganishwa na muda kama huo mwaka jana 2021.

Mfumuko wa bei na kupanda gharama za maisha ni mgogoro wa pili kwa ukubwa hivi sasa Uingereza baada ya mgogoro wa nishati

 

Mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa pamoja na kupanda vibaya gharama za maisha huko Uingereza, zimeitumbukiza nchi hiyo katika kipindi kigumu mno cha kiuchumi ambacho hakijawahi kutokea huko Uingereza katika muda wa nusu karne iliyopita.

Mfumuko huo wa bidhaa unaoshuhudiwa huko Uingereza unatokana na kujitoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya maarufu kwa jina la Brexit, mgogoro wa UVIKO-19 yaani corona pamoja na  vita vya Ukraine ambavyo vimesababisha gharama za maisha kupanda kwa asilimia 60 huko Uingereza.

Hivi karibuni Rais Vladimir Putin wa Russia alisema kuwa, vikwazo vya Magharibi dhidi ya Moscow kabla ya kusababisha matatizo kwa Russia vinazisababishia matatizo mengi nchi tofauti duniani zikiwemo nchi za Magharibi zenyewe, ukiwemo upungufu wa chakula na mfumuko wa bei za bidhaa muhimu na za dharura.