May 25, 2022 08:27 UTC
  • Indhari; hali mbaya kabisa ya uchumi wa dunia kuwahi kushuhudiwa tangu Vita vya Pili vya Dunia

Baada ya miaka miwili ya msambao wa maradhi ya Covid-19 pamoja na matokeo mabaya yaliyosababishwa na janga hilo na katika hali ambayo, mataifa mbalimbali yalikuwa katika mkakati wa kuboresha uchumi, kutokea vita vya Ukraine na Russia kumevuruga zaidi hali ya uchumi wa dunia.

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Kimataifa wa Fedha IMF ametoa indhari kuhusiana na kuongezeka mfumuko wa bei na kudorora uchumi duniani kote. Kristalina Georgieva ametoa indhari hiyo katika hotuba ya hafla ya ufunguzi wa mkutano wa Jukwaa la Dunia la Uchumi huko mjini Davos, Uswisi.

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa IMF ameeleza kuwa, kutokana na janga la dunia nzima la virusi vya corona, vita vya Ukraine na mabadiliko ya tabianchi, nchi za ulimwengu zimekumbwa na ughali wa bidhaa na uzorotaji wa uchumi ambao haujawahi kushuhudiwa.

Georgieva ameongeza kuwa, "tangu wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia hadi sasa, uchumi wa dunia uko kwenye hali mbaya zaidi na unakabiliwa na mazingira magumu mno."

Kuenea kwa maradhi ya Covid-19 na kubakia kwa muda mrefu watu katika karantini na vilevile kulazimika mataifa ya dunia kuweka bajeti kubwa kwa ajili ya sekta ya afya na dawa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ni mambo ambayo kwa hakika yamepunguza uzalishaji na wakati huo huo, kuongeza ukosefu wa ajiira na kufilisika sehemu kubwa ya sekta za uzalishaji.

Hali hii imekuwa na taathira hasi kwa uchumi wa mataifa mengi kiasi kwamba, hata mataifa yenye uchumi mkubwa na imara wa viwanda kama Ujerumani nayo yameathirika na hali hii.

Wakimbizi nchini Afghanistan

 

David Malpass, Rais wa Benki ya Dunia sambamba na kusisitiza udharura wa kuchukuliwa hatua zenye uratibu wa kimataifa na majimui ya sera jumla za kitaifa amesema: Kuongezeka ukosefu wa usawa na hatari za kiusalama kutakuwa na madhara kwa dunia hususan kwa nchi zilizoko katika mkondo wa kustawi.

Katika upande mwingine, mabadiliko ya tabianchi na vilevile kupuuza mataifa makubwa kama Marekani suala la uchafuzi wa mazingira, ni sababu nyingine inayotajwa na wajuzi wa mambo kwamba, imekuwa na taathira katika kupanda gharama za maisha na kupungua ustawi wa uchumi ulimwenguni. Utafiti uliofanywa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa katika uwanja huu unaonyesha kuwa, hadi kufikia mwaka 2050 maisha ya mwanadamu katika mgongo wa ardhi yatabadilika.. Hiii ni kutokana na matokeo haribifu ya mabadiliko ya tabianchi kama ukame na njaa.

Wataalamu hao wanaonya kuhusiana na matokeo haribifu ya mabadiliko ya tabianchi kwa kusema, kuongezeka joto duniani kwa zaidi ya nyuzijoto 1.5 kutapelekea kuibuka taathira zisizoweza kufidika  kwa mfumo wa maisha ya mwanadamu pamoja na mazingira anayoishi.

Licha ya kuwa, akthari ya serikali na tawala duniani zimetia saini hati ya makubaliano ya Paris ya mwaka 2015 na kuahidi kufungamana nayo kwa kufanya juhudi za kuhakikisha zinasaidia kupunguza kiwango cha joto duniani, lakini hakuna kilichofanyika katika uwanja huo.

Hii ni katika hali ambayo, wataalamu wa mambo wanasema kuwa, endapo hilo halitafanikiwa, watu wapatao bilioni 3 na milioni 500 duniani watabakia bila makazi katika kipindi cha miaka 50 ijayo, sababu kuu ikiwa ni mabadiliko ya tabianchi na madhara kwa uchumi yatakuwa makubwa pia.

Kristalina Georgieva Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF) 

 

Katika hali ambayo, mataifa mbalimbali ya dunia yamo katika harakati za kuandaa mikakati ya kiuchumi kwa ajili ya kuvuka kipindi hiki cha mgogoro wa kiuchumi uliotokana na janga la Covid-19, kuanza kwa vita vya Russia na Ukraine kumezidi kuharibu hali ya mambo na uchumi wa dunia. Shirika la Biashara Duniani (WTO) linatabiri kuwa, vita vya Russia na Ukraine vinaweza kupunguza kwa asilimia 50 ukuaji wa biashara duniani katika mwaka huu wa 2022 huku ukuaji wa uzalishaji wa ndani wa mali ghafi nao ukitarajiwa kupungua mno.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo ni kuwa, licha ya kuwa hisa ya Russia na Ukraine katika biashara yote duniani na uzalishaji duniani ni ndogo, lakini mataifa hayo mawili ni wazalishaji na wadhamini wa bidhaa muhimu na za dharura hususan chakula na nishati.

Filihali, Kristalina Georgieva Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Kimataifa wa Fedha (IMF) anazitaka nchi tajiri zipunguze vizuizi vya kibiashara na kuboresha mifumo ya kifedha ya nje ya mipaka yao, ili kuzisaidia nchi dhaifu nazo zikue na kustawi kiuchumi.

Mkuu huyo wa IMF anaeleza kuwa, athari za kupanda kwa bei za bidhaa za chakula na nishati ni kubwa mno kwa familia na akaongezea kwa kusema: "Hali hii mbaya imesababisha matatizo mengi kwa nchi za ulimwengu wa tatu, hivyo zinahitaji kusaidiwa."

Inaonekana kuwa, katika hali ya hivi sasa indhari zinazotolewa katika uwanja huu zinapaswa kuzingatiwa na kupewa uzito maalumu.