May 26, 2022 03:35 UTC
  • ICC yatakiwa ichunguze uhalifu wa kivita wa Israeli Gaza

Mashirika kadhaa ya kutetea haki za Wapalestina yameikabidhi Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) maelezo ya kina kuhusu jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa na utawala wa Israel wakati wa hujuma zake za kijeshi dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza mwaka 2021.

Mashirika ya haki za binadamu ya Palestina, ikiwa ni pamoja na al-Haq, al-Mezan, na Kituo cha Haki za Binadamu cha Palestina (PCHR), ambayo hufuatilia na kuandika ripoti kuhusu ukiukaji wa haki unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel yaliwasilisha ripoti kwa mahakama hiyo yenye makao makuu yake The Hague ili kuharakisha uchunguzi kuhusu uhalifu na ukiukaji unaofanywa na utawala wa Tel Aviv na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria.

"Shambulio la Mei 2021 huko Gaza ni mfano wa hivi karibuni zaidi wa mfululizo wa mashambulizi ya kijeshi yenye uharibifu mkubwa na yenye lengo la kusababisha uharibifu usio na uwiano na mateso kwa raia wa Ukanda wa Gaza, eneo ambalo linakabiliwa na mzingiro unaotekelezwa na Israel kinyume cha sheria kwa muda wa miaka 15,” alisema Raji Sourani, Mkurugenzi wa PCHR.

Tel Aviv ilianzisha kampeni ya kikatili ya kuushambulia Ukanda wa Gaza mnamo Mei 10, 2021, kufuatia hatua za kulipiza kisasi za Wapalestina kufuatia uvamizi wa kikatili uliotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya waumini wa Msikiti wa al-Aqsa na mipango ya utawala huo ya kuzilazimisha familia kadhaa za Kipalestina kuhama nyumba zao za jadi huko Sheikh Jarrah, kitongoji cha Quds (Jerusalem) Mashariki inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo dhalimu.

Uharibifu uliosababishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita vya Gaza

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, Wapalestina 260 waliuawa shahidi katika mashambulizi hayo ya Israel, ikiwa ni pamoja na watoto 66 na wanawake 40. Takriban Wapalestina  wengine 1,948 pia walijeruhiwa.

Katika kukabiliana na hujuma za Israel, harakati za mapambano ya Kiislamu au muqawama huko Palestina, zikiongozwa na Hamas, zilianzisha Operesheni ya Upanga wa al-Quds na kuvurumisha makombora zaidi ya 4,000 katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu  na kuua Waisraeli wasiopungua 12.

Israel ilishtushwa na msururu wa maroketi na makombora kutoka Gaza, na hivyo ikalazimika kutangaza usitishaji vita wa upande mmoja Mei 21, ambapo makundi ya Palestina yalikubali kusitisha mapigano kwa upatanishi wa Misri.