May 26, 2022 06:40 UTC
  • Mauaji mapya ya ufyatuaji risasi huko Marekani na radiamali ya pupa ya Biden

Katika kisa kingine cha ufyatuaji risasi dhidi ya umati nchini Marekani ambacho kimepelekea kuuawa wanafunzi wengi ya shule ya msingi, Rais Joe Biden wa nchi hiyo kama alivyofanya katika siku za nyuma, ametoa radiamali ya pupa na isiyo ya busara katika uwanja huo.

Kabla ya hapo, Biden alikuwa ameamuru bendera ya Marekani ipeperushwe nusu mlingoti katika Ikulu ya White House na majengo mengine ya umma kufuatia tukio hilo. Amesema: "Nilitarajia nisingeona jinai nyingine kama hii nitakapokuwa rais.... Ufyatuaji risasi kama huu haufanyiki sehemu nyingine yoyote duniani, lakini unafanyika Marekani kwa sababu kila mtu ana ruhusa ya kubeba silaha. Ukweli kuwa kijana mwenye umri wa miaka 18 anaweza kuruhusiwa kuingia kwenye duka la mauzo ya silaha na kununua bunduki si jambo sahihi." Alikuwa akiashiria tukio la hivi karibuni la mauaji ya wanafunzi wa shule ya msingi ambapo kijana mmoja mdogo alihusika. Kabla ya hapo kijana mwingine mweupe mwenye umri wa miaka 18 alifyatua risasi kiholela dhidi ya wateja na hasa weusi katika duka moja huko katika mji wa Buffallo katika jimbo la New York na kuwaua watu wasiopungua 10.

Siku ya Jumanne vyombo vya habari vya Marekani viliripoti ufyatuaji risasi uliotokea katika shule moja huko Uvalde, Texas. Waliofariki katika ufyatuaji risasi huo ni watu 22, 19 kati yao wakiwa ni watoto wadogo na wengine watatu watu wazima. Mshambuliaji alikuwa mvulana wa miaka 18 anayeitwa Salvador Ramos ambaye pia aliuawa. Akitoa radiamali yake kuhusiana na ufyatuaji risasi huo huko Texas, Kamala Harris Makamu wa Rais wa Marekani pia ametoa wito wa kubanwa matumizi na uuzaji wa silaha za moto nchini Marekani. Amesema: "Mioyo yetu inaendelea kuumia kutokana na ufyatuaji risasi katika shule za Marekani. Inatosha, yaani inatosha."

Matumizi ya silaha za moto Marekani ni kama kununua nyanya sokoni

Mauaji yanayotokana na matumizi mabaya ya silaha, na ambayo ni mojawapo ya matatizo sugu zaidi nchini Marekani yanaendelea kuongezeka siku baada ya nyingine na sasa yametoka kabisa katika udhibiti wa serikali na polisi ya Marekani.

Wataalamu wa masuala ya usalama wanaamini kuwa kile kinachotishia usalama wa ndani wa Marekani sio ugaidi wa kimataifa wala vitisho kutoka nje, bali ni watu wenye itikadi kali za mrengo wa kulia yakiwemo magenge ya watu weupe wanaojiona kuwa bora kuliko watu wengine na pia kuenea nchini humo mienendo ya matumizi ya mabavu yakiwemo matumizi ya silaha za moto. Mojawapo ya kesi zilizoripotiwa mwaka 2021 za matumizi mabaya ya silaha na ufyatuaji risasi wa kiholela huko Marekani ni pamoja na kesi 693 za ufyatuaji risasi dhidi ya umati zilizosababisha vifo vya watu 702 na kupelekea wengine zaidi ya 2,800 kujeruhiwa.

Silaha za moto ni moja ya sababu kuu za vifo nchini Marekani. Marekani ni miongoni mwa nchi ambazo ununuzi na ubebaji silaha unafanyika kirahisi na hadharani, na kwa sababu hiyo, makampuni ya silaha yanapata faida kubwa kutokana na mauzo ya silaha mbali mbali. Kati ya silaha milioni 857 zinazopatikana kirahisi mikononi mwa raia wasiokuwa wanajeshi ulimwenguni, Wamarekani wanamiliki silaha milioni 393 kati ya hizo. Inakadiriwa kuwa kuna takriban bunduki 120 kati ya kila Wamarekani 100, silaha ambazo kwa kawaida matumizi yake huongeza kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za kisaikolojia, kitaaluma, kulipiza kisasi cha  mtu binafsi, cha kifamilia au kijamii. Wakati huo huo kuwepo silaha mikononi mwa magenge ya ubaguzi wa rangi na yenye mielekeo ya itikadi kali kumeongeza kwa kiasi kikubwa matukio ya ufyatuaji risasi wa umati nchini Marekani.

Serikali za Republican, ikiwemo ya utawala wa zamani wa Trump, kimsingi haziamini kuzuia ununuzi na ubebaji silaha hadharani nchini Marekani. Katika hali ambayo serikali za Wademokrat, ikiwa ni pamoja na serikali ya zamani ya Barack Obama na ya sasa ya Joe Biden, kidhahiri zimekuwa zikifuatilia marekebisho ya sheria ya kubana matumizi ya bunduki katika jamii, lakini wamiliki wa makampuni makubwa ya kutengeneza silaha yenye ushawishi mkubwa  katika Congress wamezui kabisa kuwekwa vikwazo katika manunuzi na ubabeji wa bunduki hadharani nchini humo.

Kwa hakika, faida kubwa inayotokana na mauzo ya silaha za moto imeyapelekea makampuni ya silaha kutumia lobi zao zenye nguvu katika Congress kwa ajili ya kuzuia kupitishwa na kutekelezwa sheria zozote zinazohusiana na kuzuia ununuzi na ubebaji silaha usio wa kuwajibika nchini.

Mauaji yanayotokana na ubebaji silaha hadharani ni jambo la kawaida Marekani

Watu wengi nchini Marekani wanaamini kuwa uzembe wa serikali za Marekani na Bunge la Congress kuhusu suala zima la kubeba silaha na kubuni sheria katika uwanja huo ndio sababu kuu ya kuendelea msururu wa mauaji yanayotokana na ufyatuaji risasi wa kiholela nchini humo.  Jambo la kusikitisha ni kuwa kila mara matukio ya mauaji ya aina hayo yanapotokea, viongozi wa Marekani na hasa marais, husisitiza juu ya haja ya kupitishwa sheria za kudhibiti ubebaji na matumizi ya bunduki, lakini baada ya muda kila kitu husahaulika na hali ya kawaida kuruhusiwa kuendelea. Kwa hakika, serikali ya Marekani ambayo inadai kurekebisha hali inayotawala duniani na hivyo kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine yenyewe imeshindwa kutatua moja ya masuala ya kimsingi kabisa yanayohusiana na usalama wa raia wake.

Tags