May 26, 2022 10:38 UTC
  • Kissinger: Kufeli mazungumzo ya Russia na Ukraine kutakuwa na madhara makubwa kwa Ulaya

Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani amesema kuwa, kufeli juhudi za kuitisha mazungumzo baina ya Ukraine na Russia kutakuwa na madhara makubwa ya muda mrefu kwa nchi za Ulaya.

Tangu vilipoanza vita vya Russia na Ukraine tarehe 24 Februari mwaka huu, kumeshaitishwa mazungumzo kadhaa ya ngazi tofauti baina ya pande hizo mbili lakini yote yameshindwa kusimamisha vita hivyo.

Hata mazungumzo baina ya mawaziri wa mambo ya nje wa Russia na Ukraine yaliyofanyika nchini Uturuki, nayo hayakuzaa matunda yoyote.

 

Gazeti la New York Times limemnukuu Henry Kissinger, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani akisema kwenye Kongamano la Kimataifa la Uchumi huko Davos Uswisi kwamba, kuna haja na kuongezwa jitihada za kuhakikisha mazungumzo baina ya pande hizo mbili yanafanyika haraka katika kipindi kisichozidi miezi mwili ijayo kabla ya vita vya Ukraine havijaleta madhara makubwa zaidi.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa zamani wa Marekani pia amesema, anavyoona yeye ni kwamba kupewa Russia baadhi ya ardhi ya Ukraine kunaweza kumaliza vita hivyo.

Baada ya kutolewa pendekezo hilo na waziri huyo wa zamani wa Marekani, mbunge wa Ukraine, Inna Sovsun ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "Inasikitisha kuona kuwa waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani anaamini kuwa kukabidhi kwa nchi nyingine ardhi ya nchi huru ndiyo njia ya kupatikana amani kwa kila nchi."