May 27, 2022 02:32 UTC
  • Imran Khan aipa serikali ya Pakistan siku sita kuvunja mabunge na kutangaza uchaguzi mpya

Aliyekuwa waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan, ametoa onyo kwa serikali kwamba ama itangaze uchaguzi mpya katika muda wa siku sita zijazo au ataongoza tena maandamano ya mamilioni ya watu katika mji mkuu Islamabad.

Khan ametoa muhula huo alipohutubia maandamano ya maelfu ya wafuasi wake jana Alkhamisi mjini Islamabad ambayo lengo lake ni kuipigisha magoti serikali na kulazimisha kuitishwa uchaguzi wa mapema.

"Nilikuwa nimeamua niketi hapa mpaka serikali iyavunje mabunge na kutangaza uchaguzi, lakini kutokana na niliyoyaona katika masaa 24 yaliyopita, inaonyesha wameamua kulilelekeza taifa kwenye hali ya mchafukoge", amesema mwanasiasa huyo akinukuliwa na tovuti ya habari ya Dawn.

Serikali ya waziri mkuu Shehbaz Sharif ilichukua hatua mapema za tahadhari kwa kusambaza askari wa kulinda majengo muhimu yakiwemo ya bunge na ofisi za rais na waziri mkuu huyo. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kuzuka mapigano baina ya polisi na wafuasi wa Khan.

Imran Khan akihutubia wafuasi wake

Katika hotuba hiyo aliyotoa mbele ya wafuasi wake, waziri mkuu wa Pakistan aliyeuzuliwa na bunge kwa kura ya kutokuwa na imani naye amedai kuwa, wafuasi wake watano wameuawa katika ghasia zilizotokea kwenye maeneo mbalimbali ya nchi, hata hivyo serikali haijatoa maelezo yoyote kuhusiana na madai hayo ya Khan.

Mapema kabla ya hapo, Imran Khan alikuwa ameapa kwamba atafanya mgomo wa muda mrefu wa kuketi hadi ahakikishe matakwa yake yamekubaliwa.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 69 ambaye aliondokea kuwa mchezaji wa kriketi, alishikilia wadhifa wa uwaziri mkuu wa Pakistan kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu kabla ya kuondolewa mwezi uliopita wa Aprili kwa kura za wabunge za kutokuwa na imani naye.

Tangu wakati huo, Imran Khan amekuwa akiitisha mikutano nchi nzima na kutangaza kuwa kuondolewa kwake madarakani ni matokeo ya njama iliyoongozwa na Marekani kwa kushirikiana na Shehbaz.

Maandamano ya Khan na wafuasi wake kuelekea mji mkuu Islamabad yalianzia Peshawar, mji ulioko kaskazini-mashariki ya Pakistan.../

Tags