May 27, 2022 02:33 UTC
  • Seneta wa Marekani akiri kuhusu dhulma za kihistoria ambazo nchi yake imeifanyia Iran

Seneta Tim Kaine wa jimbo la Virginia amekiri kuwa matukio kadhaa ya kihistoria yamechangia kuifanya Iran isiwe na imani na Marekani.

Akizungumza katika kikao cha kamati ya uhusiano wa nje ya Seneti, kilichohudhuriwa na mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran Robert Malley, Tim Kaine amesema, "kwa mtazamo wa Wairan, Marekani ni hatari na haiaminiki. Marekani ilisaidia kuiangusha serikali ya waziri mkuu wa Iran (serikali ya Dakta Musaddiq) mwaka 1953. Marekani ilichangia kumweka madarakani Shah wa Iran; mtu ambaye kwa muda wa miaka 20 aliwatawala kidikteta watu wa Iran. Wakati Shah alipopinduliwa, kinyume na ushauri iliopewa na wizara ya mambo ya nje, Marekani ilimpa hifadhi, hatua ambayo ilipelekea kushikiliwa ubalozi wa Marekani (kutekwa Pango la Ujasusi)."

Dikteta Shah aliyerejeshwa madarakani na Marekani kupitia mapinduzi ya kijeshi ya 1953

Seneta huyo wa Virginia ameendelea kubainisha msaada wa Marekani na uungaji mkono wake kijeshi kwa Iraq katika Vita vya Kulazimisha ilivyoanzisha dhidi ya Iran na akasema, Washington ilichangia hata kuuliwa raia wa Iran kwa silaha za kemikali.

Kutunguliwa kwa kombora la manowari ya Marekani ndege ya abiria ya Iran kulikosababisha kuuawa raia wake wapatao 300 waliokuwa wameabiri katika ndege hiyo, ni nukta nyingine iliyoashiriwa na Seneta Kaine.

Katika kikao hicho cha kamati ya mambo ya nje ya Seneti ya Marekani, Robert Malley, mjumbe maalumu wa White House katika masuala ya Iran alikiri kuwa Iran inaitumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani na akaongeza kwamba, kama serikali iliyopita ilivyokiri wakati inajitoa kwenye makubaiano ya JCPOA, Iran ilikuwa imeheshimu na kutekeleza ahadi na majukumu yake.

Katika siku za karibuni, suala la kuyafufua makubaliano ya nyuklia limekuwa likizungumziwa zaidi ndani ya Marekani kuliko wakati mwingine wowote.../