May 28, 2022 03:24 UTC
  • Kulaaniwa mauaji ya Waislamu wa Kishia Afghanistan

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa wa hali ya haki za binadamu nchini Afghanistan amelaani mauaji ya Waislamu wa Kishia wa jamii ya Hazara nchini humo; na mbali na kubainisha kwamba mauaji hayo yanayoilenga jamii hiyo yameratibiwa kwa mpangilio maalumu ametahadharisha pia juu ya matokeo mabaya ya hujuma hizo.

Baada ya ziara yake ya Afghanistan, Richard Bennett ameeleza katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari katika mji mkuu wa nchi hiyo Kabul kwamba mauaji ya Mashia ni "jinai dhidi ya binadamu".

Richard Bennett

Katika mauaji ya kigaidi ya hivi karibuni yaliyofanywa katika mji wa Mazar Sharif, ambayo kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) limetangaza kuwa ndilo lililohusika, makumi ya watu wameuawa na kujeruhiwa. Ripota huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa ametoa tamko hilo kuhusiana na mauaji hayo katika hali ambayo duru za Magharibi zinazojigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu zingali zimenyamaza kimya na zinatazama tu wananchi wa Afghanistan wanavyoendelea kuuawa. Marekani ndio inayojulikana kuwa msababishaji mkuu wa maafa hayo kwa hatua yake ya kuwahamisha magaidi wa Daesh kutoka Syria na Iraq na kuwapeleka Afghanistan na kuyaimarisha makundi ya kigaidi na ya wanamgambo ndani ya nchi hiyo.

Magaidi wa kundi la DAESH(ISIS) nchini Afghanistan

Samia Moruvati, mtaalamu wa masuala ya kisiasa analielezea hilo kama ifuatavyo: "Baada ya kushindwa Daesh, Marekani ilianzisha fitna mpya Afghanistan kwa kuwahamishia nchini humo magaidi wa kundi hilo ili kuitumbukiza Afghanistan yenyewe kwenye wimbi jipya la mapigano na machafuko na pia kuyumbisha amani ya eneo."

Baadhi ya duru za kisiasa za kikanda zinazopokea taarifa kutoka ndani ya Afghanistan zinaeleza kuwa, kuendelea kuwapo tofauti baina ya mirengo miwili ya Haqqani na Mullah Baradar kwa upande mmoja, na kushindwa kukidhiwa wanachama wa Taliban matakwa yao wa kifedha na ya nyadhifa za kijeshi na kisiasa kwa upande mwingine, kumewafanya baadhi ya wanachama hao wajitoe katika kundi hilo na kujiunga na Daesh; na kwamba wanachama hao wa Taliban wamechangia na kuhusika katika kushadidisha mashambulio ya kigaidi hasa yanayofanywa kwa uratibu na malengo maalumu.

Inasemekana kuwa, kundi la Haqqani lingali linafanya kazi likiwa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Shirika la Intelijensia la Jeshi la Pakistan ISI na kwa sababu hiyo linakwamisha kutekelezwa makubaliano ya Doha baina ya mrengo wa Taliban wa Mullah Baradar na Marekani. Na kwa kutumia kisingizio hicho, Washington nayo imeamua kuzuia mali za Afghanistan na kuwaunga mkono wapinzani wa Taliban, jambo ambalo limeshadidisha machafuko ya umwagaji damu nchini humo.

Kuhusiana na suala hilo, Ali Khazai, mtaalamu wa masuala ya Pakistan anasema: "moja ya nukta ambazo zinaangaliwa kwa uzito mdogo ni kuendelea kuwepo tofauti kati ya mirengo miwili ya Taliban, yaani wa Haqqani na wa Mullah Baradar, hasa katika mkoa wa Nangarhar mashariki mwa Afghanistan, mahali ambapo kundi la kigaidi la Daesh linapachukulia kuwa ndio ngome yake; na kwa kutoa ahadi mbalimbali za kilaghai linawavutia wanachama wa Taliban wasioridhishwa na kundi hilo, huku likichochea machafuko nchini Afghanistan kwa ajili ya kufanikisha malengo yake maovu na ya kuzusha mifarakano nchini humo.

Hujuma ya mauaji ya Waislamu wa Kishia ndani ya msikiti

Alaa kulli haal, wananchi wa Afghanistan wana matarajio kwa Umoja wa Mataifa kwamba utawasaidia kutatua matatizo yanayowakabili kulingana na majukumu ya kimataifa iliyonayo taasisi hiyo; na si kutosheka na kutoa ripoti tu. Sababu ni kwamba Umoja wa Mataifa, ambao ndio asasi kubwa zaidi ya kimataifa una jukumu la kuleta amani na kuzisaidia nchi wanachama kufikia lengo hilo. Kwa muktadha huo, taasisi hiyo inapaswa kutumia nyenzo na uwezo wake wote ili kukomesha machafuko ya umwagaji damu nchini Afghanistan, kwa sababu hivi sasa kuna hofu kwamba magaidi watakapopata nguvu ndani ya Afghanistan, amani na usalama wa eneo zima pia utakuwa hatarini.../

Tags