May 28, 2022 10:19 UTC
  • Trump: Waalimu Marekani wabebe silaha wakiwa darasani

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amepinga vikali mpango wowoto wa kudhibiti umiliki wa silaha nchini humo baada ya mauaji ya hivi karibuni ya watoto shuleni na badala yake ametaka waalimu wapewa haki ya kubeba silaha wakiwa darasani.

Akizugumza Ijumaa katika mkutano wa Jumuiya ya Kitaifa ya Bunduki (NRA) ambalo ni kundi lenye nguvu linalounga mkono wananchi kumiliki silaha Marekani, Trump amesema ufyatuaji risasi kama ule uliojiri Texas ni dalili kuwa wananchi hawapasi kupokonywa silaha bali wanapaswa kumiliki silaha.

Katika hujuma hiyo ya kigaidi ndani ya shule jimboni Texas siku ya Jumanne, watoto 19 na waalimu wawili waliuawa. Hii ni hujuma ya pili dhidi ya shule ya msingi nchini Marekani katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. 

Hivi karibuni pia watu 10 waliuawa na watatu kujeruhiwa katika shambulio la ubaguzi wa rangi kwenye duka kubwa huko Buffalo, New York. 

Trump ameashiria mauaji hayo ya Texas na kusema: "Sasa wakati umefika ambapo walimu waliopewa mafunzo waruhusiwe kuwa na silaha wakiwa darasani".

Hali baada ya ufyatuaji risasi kiholela katika shule jimboni Texas. Picha ya chini ni ya kijana aliyetekeleza jinai hiyo ya kigaidi

Trump ameendelea kwa kumtuhumu Rais Joe Biden wa Marekani kuwa analenga kutumia masaibu ya wengine kwa maslahi yake ya kisiasa na kuweka sheria za kubana umiliki wa silaha. Kufuatia mauaji ya shuleni jimboni Texas Biden amesema kuna haja ya kukabiliana na makundi yanayounga mkono umiliki wa silaha Marekani. Trump ni mmoja kati ya waungaji mkono wakubwa zaidi wa haki ya wananchi kumiliki silaha Marekani

Hivi karibuni televisheni ya CNN, imetangaza kuwa ripoti ya utafiti uliofanywa na taasisi moja ya Uswisi inayoshughulika na masuala ya umiliki silaha inayoitwa asasi ya "utafiti wa silaha ndogondogo" imeeleza kuwa, katika kila Wamarekani 100 kuna silaha zisizopungua 120.