May 28, 2022 10:41 UTC
  • FAO: Iran ni moja ya nchi zinazozalisha chakula kwa wingi duniani

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetangaza kuwa, Iran ina nafasi muhimu katika kilimo cha chakula duniani ambapo inashikilia nafasi ya tatu hadi ya tisa katika uzalishaji wa baadhi ya mazao.

Kwa mujibu wa  ripoti mpya ya FAO yenye takwimu za mwaka 2020, Iran ni ya tatu duniani katika uzalishaji mazao ya kilimo kama vile tende, asali, pistachio na jozi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Iran huzalisha tani milioni 1.2 za tende kwa mwaka na ni ya tatu huku nafasi za kwanza na pili zikishikiliwa na Misri na Saudia kwa utaratibu huo.

Aidha kila mwaka Iran kuzalisha tani elfu 80 za asali na hivyo baada ya China na Uturuki inashika nafasi ya tatu duniani.

Hali kadhalika FAO imetangaza kuwa, mwaka 2020 Iran ilizalisha tani 190 za pistachio na hivyo kuifanya kuwa ya tatu duniani baada ya Marekani na Uturuki katika zao hilo.

Kabla ya hapo Iran ilikuwa ya kwanza duniani katika uzalishaji wa pistachio lakini ilishuka na kuwa ya tatu kutokana na ukame.

Hali kadhalika katika uzalishaji wa jozi, mwaka 2020 Iran ilizalisha tani 354 na hivyo kuifanya iwe ya tatu duniani katika zao hilo baada ya Marekani na China.

Iran ni ya tatu duniani katika uzalishaji jozi

Ripoti ya FAO pia imebaini kuwa katika ukulima wa tikiti maji, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ya nne duniani huku ikishika nafasi hiyo hiyo katika uzalishaji mbilinganya.

Iran inashika nafasi ya saba duniani katika ukulima wa vitunguu na tomato huku ikiwa ya nane duniani katika uzalishaji spinachi. Aidha ripoti hiyo ya FAO imebaini kuwa Iran ni ya nane duniani katika uzashaji machungwa. 

Ripoti ya FAO pia imesema Iran ni ya 12 duniani katika uzalishaji ngano ambapo mwaka 2020 ilizalisha tani milioni 15 huku China ikiongoza duniani kwa tani milioi 134 ikifuatiwa na India na Russia.

Katika kilimo cha chai Iran ni ya 12 duniani ambapo mwaka 2020 ilizalisha tani laki 84,000 huku China ikiongoza kwa uzalishaji wa tani milioni 2.97 ikifuatiwa na India na Kenya.

 

Tags