May 29, 2022 03:26 UTC
  • Kuondolewa vikwazo vya Magharibi, sharti la Moscow la kuuza chakula na mbolea nje ya Russia

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema kuwa, nchi yake haina tatizo na kuuza nje bidhaa za chakula na mbolea na kuikoa dunia na janga hilo, lakini tatizo ni kwa nchi za Magharibi zilizoiwekea vikwazo Russia na kukwamisha zoezi hilo. Amesema, iwapo nchi za Magharibi zitaondoa vikwazo, Moscow itaweza kuendelea kuuza chakula na mbolea kama zamani.

Pamoja na hayo lakini Rais wa Russia hakusema iwapo zoezi hilo la kusafrisha nje bidhaa muhimu za chakula na mbolea ni kuhusu Riussia tu au na Ukraine pia. Putin amesema hayo katika mazungumzo ya simu na siku ya Alkhamisi baina yake na Waziri Mkuu wa Italia, Mario Draghi.

Kwa vile Russia na Ukraine kwa pamoja zinadhamini asilimia 30 ya ngano na asilimia 80 ya nafaka zinazozalisha mafuta ya kupikia duniani, vita baina ya nchi hizo mbili vimeisababishia dunia matatizo makubwa sana. Si hayo tu lakini pia Russia ndiye mzalishaji mkubwa wa mbolea za kemikali ulimwenguni. Hii ina maana kwamba, vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya Russia vimepelekea kuzuka mgogoro wa kiuchumi duniani kwani bidhaa hiyo muhimu na ya kiistratijia haiwezi kuwafikia wakulima. Mgogoro huo ni mkubwa hasa kwa kuzingatia matatizo chungu nzima ya tabianchi, mazingira pamoja na taathira za janga la UVIKO-19 yaani corona. Kabla ya kuanza vita vya Ukraine pia, nchi hiyo ilikuwa msafirishaji mkubwa wa ngazo duniani pamoja na nafaka nyingine kama alizeti. Nchi nyingi duniani hasa za Afrika Kaskazini tegemeo lao kuu kwa bidhaa hizo muhimu ilikuwa ni Ukraine. Sasa hivi bidhaa hizo zimejaa kwenye maghala ya Ukraine, lakini hakuna uwezekano wa kusafirishwa nje ya nchi.

Vita nchini Ukraine

 

Wataalamu wameonya kwamba, akiba ya ngano katika maghala ya nchi mbalimbali duniani itamalizika karibuni tu hivi. Upungufu mkubwa wa mbolea za kimemikali pia ni mgogoro mwingine mkubwa pembeni mwa ukame na ukosefu wa mvua uliozikumbwa nchi nyingi duniani. Sara Menker, mkurugenzi wa "Gro Intelligence" anasema, ukosefu wa usalama wa chakula duniani ni mkubwa sana hivi sasa na haujawahi kushuhudiwa mfano wake tangu dunia ilipokumbwa na mgogoro wa fedha mwaka 2008. Mtaalamu huyo amesema katika ripoti yake kwa Umoja wa Mataifa kwamba, akiba ya ngano hivi sasa duniani inatosha kwa muda wa wiki 10 tu zijazo. Mtaalamu huyo amesema hayo mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa: Vita baina ya Russia na Ukraine si sababu ya mgogoro huo, bali sababu yake hasa ni vita ambavyo moto wake unawaka kwa muda mrefu.

Hivi sasa Russia na Ukraine kila moja inamtuhumu mwenzake kukwamisha usafirishaji wa bidhaa za chakula nje ya nchi hizo. Andrei Rudenko, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alisema siku ya Jumatano kuwa, Ukraine ndiyo inayopaswa kulaumiwa kwa kukwama usafirishaji nje wa bidhaa za chakula na nafaka kwani imetega mabomu kwenye bandari. Ukraine inapinga madai hayo na kusema kuwa, Moscow hairuhusu meli kutia nanga kwenye bandari za Ukraine. Andrei Ruderinko amesema: Russia haina tatizo na suala la kufungua njia ya kutoka meli za chakula huko Ukraine, lakini tatizo ni vikwazo na iwapo baadhi tu ya vikwazo hivyo vitaondolewa, Moscow itakuwa tayari kufungua njia hizo.

Dunia hivi sasa iko kwenye mgogoro mkubwa wa nafaka kutokana na vikwazo vya Magharibi na vita vya Ukraine

 

Kiujumla ni kwamba, nchi za Magharibi zimeiwekea Russia vikwazo vikubwa mno mpaka kwenye masuala ya michezo, kwa kisingizio cha vita vya Ukraine. Vikwazo hivyo zimesababisha matatizo makubwa ulimwenguni hasa upande wa vyakula vya nafaka kama ngano na pia nafaka za kuzalisha mafuta ya kupikia, kama alizeti.

Kiujumla ni kwamba vikwazo hivyo vikubwa vya nchi za Magharibi ambavyo havijawahi kuwekwa katika historia ya Russia, vimeilazimisha Moscow kujibu ikiwa ni pamoja na kuzuia kupeleka bidhaa zake kwa nchi ambazo si rafiki. Sasa hivi pia, Rais Vladimir Putin amesema sharti la Russia la kupeleka bidhaa zake ambazo kwa hakika ni muhimu mno kwa nchi zote za duniani, ni kuondolewa vikwazo ilivyowekewa na nchi za Magharibi. Kwa kuzingatia hayo tunaweza kusema kuwa, mkwamo wa kuweza kuzifikia nchi za dunia bidhaa muhimu na za kimsingi za chakula utaendelea kuwepo na jambo hilo hilo haliashirii kitu kingine isipokuwa kumbwa dunia na mgogoro mkubwa zaidi wa chakula kuwahi kutokea ulimwenguni.

Tags