Jun 07, 2022 10:48 UTC
  • Radiamali mbalimbali kuhusiana na hatua ya baadhi ya viongozi wa chama tawala nchini India ya kumvunjia heshima Mtume SAW

Matamshi ya utovu wa adabu ya viongozi wawili wa chama tawala nchini India cha Bharatiya Janata (BJP) dhidi ya Bwana Mtume (SAW) yamekabiliwa na wimbi la malalamiko ya mataifa ya Kiislamu na Waislamu kwa ujumla ulimwenguni.

Kufuatia matamshi hayo ya kumvunjia heshima Bwana Mtume (SAW) baadhi ya nchi ikiwemo Iran, Kuwait na Qatar zimewaita mabalozi wa India katika nchi hizo na kuwapatia malalamiko yao ambapo sambamba na kulaani kitendo hicho zimeitaka serikali ya New Delhi ichukue hatua za kukabiliana na hatua yoyote inayovunjia heshima thamani na matukufu ya dini ya Kiislamu.

Msemaji wa jeshi la Pakistan amelaani vikali matamshi ya kumvunjia heshima Mtume (SAW) yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa chama tawala nchini India na kusema kuwa, serikali ya India inajihusisha na vitendo vya kujeruhi hisia za dini za walio wachache na kushadidisha chuki dhidi ya jamii ya Kiislamu.

Kwa upande wake Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Pakistan imemuita balozi mdogo wa India mjini Islamabad na kumkabidhi malalamiko yake na ya wananchi wa Pakistan kuhusiana na kuenezwa mchezo mchafu wa chuki na propaganda dhidi ya Uislamu nchini India hususan matamshi ya kifidhuli  ya maafisa wawili wa chama tawala nchini India

Zabihullah Mujahid, msemaji wa serikali ya Taliban nchini Afghanistan amelaani kwa maneno makali katika ujumbe wake kwenye mtandao wa twitter matumizi ya maneno ya utovu wa adabu ya afisa wa ngazi za juu wa chama tawala nchini India dhidi ya Bwana Mtume (SAW).

 

Kwa upande wake Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu  (OIC) imetoa taarifa na kulaani vikali matamshi hayo ya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW na kusema, yamekuja huku kukishuhudiwa kuongezeka chuki na uhasama dhidi ya Uislamu nchini India na ukandamizaji Waislamu nchini humo.

Chuo Kikuu cha Kiislamu ya al-Azhar cha nchini Misri nacho kimelaani utovu wa adabu wa wanachama wawili wa chama tawala cha BJP cha kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.

Chuo Kikuu cha al Azhar kimetoa taarifa nzito na yenye maneno makali ya kulaani utovu wa adabu uliofanywa na wanachama hao waandamizi wa chama tawala cha BJP cha India na kusisitiza kuwa, vitendo kama hivyo ni mfano wa wazi wa ugaidi ambao lengo lake ni kuitumbukiza dunia nzima katika vita angamizi.

Kwa upande wake Harakati ya Ansarullah ya Yemen kupitia msemaji wake   Muhammad Abdul-Salam, nayo imelaani kitendo hicho na kueleza kwamba, kumvunjia heshima Bwana Mtume SAW ni ishara ya wazi ya kufilisika kimaadili.

Naveen Kumar Jindal na Nupur Sharma ni wanachama wa BJP India waliomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW

 

Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya India imechukua hatua za kutaamaliwa na kutafakariwa kuhusiana na Waislamu na thamani za Kiislamu kama vile kubinya marasimu na shughuli za kidini za Waislamu, kupiga marufuku utoaji wa uraia kwa wahajiri Waislamu, kuondoa mamlaka ya kujitawala Kashmir na kunyamazia kimya vitendo vya ukatili na utumiaji mabavu vya wahindu wenye misimamo ya kufurutu ada dhidi ya Waislamu.

Mwenendo huu umepelekea kushadidi na kuchukua wigo mpana mno chuki dhidi ya Waislamu nchini India. Hatua za baadhi ya wahindu wenye misimamo ya kufurutu mpaka ya kuchoma moto msikiti mmoja katikati mwa India juma lililopita ni sehemu tu ya matokeo  ya siasa za chama tawala cha BJP nchini humo zinazolenga kuimarisha muelekeo wa utaifa katika nchi hiyo dhidi ya jamii ya Waislamu.

Ukweli wa mambo ni kuwa, matamshi ya utovu wa adabu ya viongozi wawili wa India dhidi ya Mtume wa rehma ni ishara ya utendaji wa chama tawala cha BJP katika kupanda mbegu za fakachi, fitina na mifarakano baina ya wafuasi wa dini mbalimbali. Wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, utumiaji mabavu na machafuko ya kidini  ambayo hutokea mara kwa mara nchini India chimbuko lake ni utendaji kama huu wa chama tawala nchini humo.

Radiamali kali zilizoshuhudiwa katika mataifa ya Kiislamu na Waislamu kwa ujumla ulimwenguni kwa matamshi ya kumvunjia heshima Mtume (SAW) licha ya kuwa yamepelekea kuuzuliwa viongozi hao katika nyadhifa zao kama ilivyodai serikali ya New Delhi, lakini matarajio ya jamii ya Waislamu nchini India na Waislamu kwa ujumla ni kuiona serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi ikichukua mkondo wa kubadilisha utendaji wake ulio dhidi ya Waislamu ambao ni wafuasi wa dini za walio wachache nchini humo na kujiepusha kabisa na vitendo vya kupigia upatu muelekeo wa utaifa.

Tags