Jun 09, 2022 12:20 UTC
  • Polisi ya Taliban Afghanistan yaanza kuajiri askari wanawake

Maafisa wa Idara ya uajiri katika jeshi la polisi la mkoa wa Balakh nchini Afghanistan wamesema jeshi hilo limeanza kuandikisha wanawake watakaoajiriwa kuhudumu kama askari.

Taliban, ambayo baada ya kushika tena hatamu za utawala nchini Afghanistan Agosti 2021 ilianzisha kampeni ya kutoa mbinyo kwa tabaka la wanawake, sasa imelegeza msimamo na kuonyesha ulainifu katika suala hilo baada ya kuruhusu wanawake waendelee na masomo na kufanya kazi. Katika hatua mpya na ya karibuni, mamlaka za mkoa wa Balkh zimetangaza uamuzi wa kuwaajiri wanawake katika idara ya polisi ya mkoa huo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Moulavi Baz Muhammad Huzaifah, kamanda wa kitengo cha ajira cha polisi ya mkoa wa Balkh ametangaza leo kuwa, kwa idhini iliyotolewa na viongozi waandamizi wa Taliban kitengo hicho kimewaajiri wanawake 143 watakaofanya kazi katika polisi ya mkoa huo.

Viongozi wa Taliban

Wakati huohuo Hussein Naderi, mtaalamu wa masuala ya kijamii katika mji wa Mazar-i-Sharif, makao makuu ya mkoa wa Balkh, ameliambia shirika la habari AVA kuwa kufanya kazi wanawake katika jeshi na polisi ni jambo la dharura kwa nchi hiyo na akasema, Taliban imechukua hatua mwafaka na sahihi kwa kuwaajiri wanawake katika jeshi la Polisi.

Wakazi kadhaa wa Mazar-i-Sharif wamekaribisha uamuzi wa kuajiriwa wanawake katika jeshi la polisi na kueleza kwamba kuwepo wanawake katika idara ya polisi kuna faida kubwa hususan kwenye kitengo cha upekuzi wa nyumba na utiaji nguvuni wanawake wahalifu.../

Tags