Jun 12, 2022 02:33 UTC
  • Kuendelea vitendo visivyo vya kibinadamu vya madola ya Ulaya dhidi ya wahajiri

Baada ya serikali ya Uingereza kuchukua uamuzi wa kuwahamishia nchini Rwanda wakimbizi wanaoomba hifadhi nchini Uingereza, sasa mahakama ya nchi hiyo nayo imeunga mkono na kuidhinisha uamuzi huo.

Jonathan Swift, Jaji wa Mahakama Kuu ya Uingereza ametangaza kuwa, kwa mujibu wa manufaa ya umma ni muhimu kwa Waziri wa Mambo ya Ndani aweze kutekeleza agizo linalohusiana na kudhibiti uhajiri.

Madola ya Ulaya katika miaka ya hivi karibuni hususan baada ya kushadidi vita baridi na kuongezeka hali ya mchafukoge katika eneo la Asia Magharibi, yamekumbwa na mgogoro mkubwa wa wahajiri ambao umekuwa ukiongezeka siku baada ya siku.

Jambo hilo limeyatafanya mataifa hayo yafumbie macho nara zao za masuala ya utu na ubinadamu na hivyo kufuata mkondo tofauti na usio wa kibinadamu ambapo kuwahamishia katika nchi ya tatu barani Afrika wahajiri wanaoomba hifadhi katika nchi zao ni miongoni mwa mikakati ya nchi hizo za bara Ulaya. Hivi karibuni serikali ya London ilitangaza kuwa, ina mpango wa kuwahamishia nchini Rwanda wakimbizi wanaoomba hifadhi nchini Uingereza. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyotiwa saini baina ya London na Kigali, watu ambao wataingia nchini Uingereza kinyume cha sheria watahamishiwa katika nchi ya Kiafrika ya Rwanda na ombi lao la ukimbizi litajadiliwa huko.

Wakimbizi wanaopinga kufurushwa Uingereza wakiwa nje ya Mahakama Kuu

 

Makubaliano hayo yamefikiwa baina ya serikali za Kigali na London baada ya Uingereza kushindwa kufikia makubaliano kama hayo na nchi za Kenya, Ghana na Albania. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, serikali ya Rwanda itapewa dola milioni 158 na serikali ya Uingereza katika kile ambacho London inakiita ni ushirikiano mpana wa uhamiaji na maendeleo ya uchumi.

Mpango huo wenye utata umelalamikiwa vikali na wapinzani na hata makundi ya kutetea haki za binadamu. Wapinzani wa mpango huo wanaamini kuwa, hatua hiyo ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza ina matashi ya kisiasa na iko kinyume na sheria na kwamba, kisheria waziri huyo hana mamlaka ya kuwafukuza wakimbizi wanaoingia nchini humo. Aidha wapinzani wasema kuwa, hatua ya chama cha Wahafidhina nchini Uingereza ya kuwasilisha mpango huo, nia yake ni kuzipotosha fikra za waliowengi kuhusiana na kashfa za hivi karibuni ndani ya chama hicho.

Katika upande mwingine wapinzani wa mpango huo wanasema, madai ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza kwamba, Rwanda ni mahali salama na penye amani hayana ukweli hasa kwa kuzingatia hali ya haki za binadamu katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Sonya Sceats, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Freedom From Torture anasema: Nimekata tamaa, lakini ninaamini kwamba, mapambano hayajafikia ukingoni na tutatumia kila wenzo kwa ajili ya kuhitimisha mwenendo huu.   

Wakimbizi wa Ukraine

 

Muamala wa chuki dhidi ya Wahajiri unafanywa na madola ya Ulaya katika hali ambayo, mataifa hayo ni kinyume kabisa na madai yao kwamba, yanaheshimu masuala ya kibinadamu na kwamba, yanaheshimu haki za binadamu. Kivitendo yamekuwa yakiamiliana na wahajiri kinyume kabisa na utu na ubinadamu. Hali hiyo iko wazi mno kiasi kwamba, hivi karibuni Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) alitahadharisha kuhusiana na hali ya wakimbizi na wahajiri katika mipaka ya Ulaya na kusema kuwa, kile kinachotokea katika mipaka ya mataifa hayo ya Ulaya kwa hakika hakikubaliki si kisheria wala kiutu na kimaadili.

Pamoja na hayo, suala la wahajiri halijageuka na kuwa tatizo kwa Uingereza tu sambamba na kuendelea vita vya Russia na Ukraine bali suala hilo limekuwa tatizo kubwa kwa bara zima la Ulaya. Viongozi wa Ulaya wamefikia makubaliano ya kutekeleza sera za pamoja kuhusiana na wahajiri na mkakati wa kugawana wahajiri wanaoingia barani humo kupitia Bahari ya Mediterania.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zinaweza kuchagua njia moja mbele ya njia mbili: Njia ya kwanza ni kuwapokea wahajiri na njia ya pili ni kuyasaidia kifedha mataifa ambayo yanawapokea wakimbizi hao.

Wimbi la wakimbizi barani Ulaya limeongezeka baada ya kuanza vita vya Russia na Ukraine

 

Nancy Faeser, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani anasema kuhusiana na jambo hili kwamba: Mataifa 12 yapo tayari kuwapokea wahajiri wanaoingia katika ardhi ya Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania ambapo Romania na Bulgaria ni miongoni mwa mataifa hayo.

Pamoja na hayo, Gerhard Karner, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Austria sambamba na kukosoa uamuzi huu wa Ulaya anataka kuweko usimamizi zaidi katika mipaka ya Umoja wa Ulaya na anasema kuwa, kuunga mkono sera za "Ulaya Iliyo Wazi" ni kutuma ujumbe wenye makosa kwa wafanya magendo.

Tags