Jun 21, 2022 07:46 UTC
  • Rais Maduro: Sisi ni sehemu ya Mrengo wa Muqawama

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema Mrengo wa Muqawama haujajibana kwa nchi fulani tu duniani, lakini unawahusu watu wote wanaopambana na ukoloni na madola ya kibeberu.

Maduro alisema hayo jana katika mahojiano maalumu na tovuti rasmi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei na kuongeza kuwa, "Mrengo wa Mapambano unapatikana kote duniani; barani Afrika, Asia, Asia Magharibi, Amerika ya Latini na hata Caribbean. "

Amesema muqawama unawahusu watu wote waliosimama kidete dhidi ya uliberali mamboleo, ubaguzi wa rangi na kijamii, na aina tofauti za ukoloni; uwe wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kimtandao.

Rais Maduro amesema: Sisi sote tunaopambana dhidi ya ukoloni, tunaopigana kwa lengo la kujikomboa kifikra na kuwakomboa watu wetu, ni sehemu ya Mrengo wa Muqawama, kambi ambayo imesimama imara dhidi ya mbinu za mabeberu wanaojaribu kuitwisha dunia ubeberu wao.

Mrengo wa Muqawama

Ameashiria njama za utawala wa Kizayuni wa Israel kupitia shirika lake la kijasusi Mossad dhidi ya Venezuela na kueleza kuwa, "Ubeberu na Uzayuni vinakula njama dhidi ya mchakato endelevu wa mapinduzi, unaoshuhudiwa Amerika ya Latini na Caribbean, na hususan Mapinduzi ya Kibolivar."

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameongeza kuwa, Mossad inapanga njama nyingi dhidi ya Caracas kutokana na msimamo wa taifa hilo la Amerika ya Latini kusimama na watu wa Palestina na kuunga mkono mapambano yao.

Tags