Jun 23, 2022 03:45 UTC
  • Makumi ya wakimbizi wa Iraqi wameripotiwa kuuawa kwa siri nchini Poland

Kamati ya Uchunguzi ya Belarus imeripoti kuwa wanajeshi wa Poland wamewaua na kuwazika kwa siri wakimbizi 135 wa Iraq.

Televisheni ya Al-Mayadin imeripoti kuwa, Kamati ya Uchunguzi ya Belarusi imekutana na wajumbe wa Iraqi huko Minsk na kuwasilisha habari ya mauaji ya halaiki na mazishi ya siri ya wakimbizi 135 wa Iraqi yaliyofanywa na wanajeshi wa Poland katika eneo la mpakani.

Kamati ya Uchunguzi ya Belarusi ilipata taarifa hizo kutoka kwa Emil Chechko, mwanajeshi wa Poland ambaye alikimbilia Belarus miezi michache iliyopita na baadaye mwili wake ukapatikana Minsk.

Ripoti zinasema maiti za wahamiaji hao wa Kiiraqi zilikuwa na majeraha kutokana na vitendo vya ukatili vya wanajeshi wa Poland.

Hali kwenye mpaka wa Belarusi na Poland imekuwa mbaya tangu Novemba mwaka jana (2021) sambamba na kuwasili maelfu ya wahamiaji kutoka Asia Magharibi nchini Belarusi.

Katika miezi ya hivi karibuni, nchi kadhaa za Ulaya zimetoa wito wa kupigwa marufuku na kuzuiwa wakimbizi wanaojaribu kuingia EU. Poland iliweka nyaya na maelfu ya askari wake kwenye mipaka ya nchi hiyo ili kukabiliana na wahajiri.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi lilisema siku ya Ijumaa iliyopita kwamba idadi ya vifo vya wakimbizi inaongezeka kwa kasi ya kutisha.

Mwaka jana zaidi ya watu 3,000 waliuawa au kutoweka katika Bahari ya Mediterania au Atlantiki wakijaribu kuvuka na kuelekea Ulaya.