Jun 23, 2022 03:49 UTC
  • Guterres aitaka jamii ya kimataifa kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Afghanistan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza masikitiko yake na kutoa mkono wa pole kwa wananchi wa Afghanistan kufuatia tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo jana Jumatano. Vilevile ameitolea wito jamii ya kimataifa kuzisaidia familia zilizokumbwa na janga hilo la kimaumbile.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa jana aliwasilisha salamu zake za rambirambi na kutoa mkoa wa taazia kwa wananchi wa Afghanistan kufuatia maafa hayo yaliyosababisha hasara za roho na mali huko Afghanistan. Amesema uwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan umejipanga kikamilifu na kwamba timu za umoja huo tayari zimeanza kutathmini mahitaji na kutoa misaada ya awali kwa waathirika wa tetemeko la ardhi.   

Idara ya Jiolojia ya Marekani imetangaza kuwa, tetemeko la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 6.1 kwa kipimo cha Rishta kulingana na mawimbi ya ndani ya ardhi, jana asubuhi liliyakumba maeneo ya kusini mashariki mwa Afghanistan na katika baadhi ya maeneo ya nchi jirani ya Pakistan. 

Imeongeza kuwa, tetemeko hilo lilitokea katika umbali wa kilomita zipatazo 44 katika mji wa Khost na katika kina cha kilomita 51. Watu wasiopungua 950 wameaga dunia kufuatia mtetemeko huo wa wa ardhi ulioikumba jana Afghanistan na mamia ya wengine wamejeruhiwa. 

Majeruhi wa tetemeko la ardhi Afghanistan wakipatiwa matibabu hospitalini 

 

Tags