Jun 23, 2022 12:10 UTC
  • New York Times: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Russia vimegonga mwamba

Chaneli ya televisheni ya Russia al Yaum imeripoti kuwa thamani ya sarafu ya Russia ya ruble imeongezeka kulinganisha na dola kwa ilivyokuwa tangu mwaka 2015 na kuongezea kwa kusema, hata gazeti la Marekani la New York Times limekiri kuwa vikwazo dhidi ya Russia vimegonga mwamba.

Wakati zaidi ya siku 100 zimepita tangu vilipoanza vita vya Ukraine, utegemezi mkubwa lilionao bara la Ulaya kwa vyanzo vya nishati vya Russia umezifanya nchi za bara hilo zikabiliwe na hali ngumu mno.

Televisheni ya Russia al Yaum imetangaza kuwa, thamani ya ruble ya Russia imeongezeka kulinganisha na sarafu za Marekani na Ulaya ambapo kwa sasa dola moja ya Marekani haifiki ruble 53 za Russia. Hii ni mara ya kwanza tangu Juni 2015 kwa thamani ya sarafu ya Russia kufikia kiwango hicho kulinganisha na dola ya Marekani.

Wakati huohuo gazetri la New York Times limeandika kuwa vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia vimegonga mwamba.

Gazeti hilo linalochapishwa Marekani limeongeza kuwa, India na China zinanunua mafuta ya Russia kwa kiwango kinachokaribiana na mafuta zinayonunua nchi za Magharibi kwa Russia. Hii ni katika hali ambayo, hivi sasa bei ya mafuta duniani imepanda, jambo ambalo limeiongezea Russia pato lake kulinganisha na miezi minne iliyopita.../