Jun 23, 2022 12:12 UTC
  • Biden akosolewa kwa kutia ulimi puani na kufumbia macho jinai za Saudia

Clare Daly, mbunge wa bunge la Umoja wa Ulaya amesema, Marekani imejihakikishia kuihodhi Ulaya kwa kuifanya soko lake jipya la gesi asilia ya LNG na wakati huohuo imelegeza msimamo kuhusu ahadi za kisiasa ilizokuwa imetoa kuhusiana na jinai za kivita za Saudi Arabia.

Mara baada ya kuingia madarakani, Rais Joe Biden wa Marekani alidai kwamba, angejikita kufuatilia masuala ya haki za binadamu nchini Saudi Arabia, lakini sasa ameamua kufanya safari ya kulitembelea eneo la Asia Magharibi na kukutana na kufanya mazungumzo na Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudia.

Clare Daly ameeleza kwamba uwezo wa Saudia wa kurubuni na kuvutia maslahi yake umeongezeka mno tangu vilipoanza vita vya Ukraine na akafafanua kwamba, katika hatua ziliyochukua kama jibu kwa Russia kwa kuanzisha vita hivyo, nchi za Ulaya ziliiwekea Moscow vikwazo kadhaa vilivyojumuisha marufuku ya kununua vyanzo vya nishati kutoka Russia, nishati ambazo zinahitajiwa mno na nchi hizo.

Clare Daly

Bi Daly ameongeza kuwa, Marekani ina hamu kubwa ya kurefusha vita vya Ukraine na kujaribu kadiri itakavyowezekana kuzuia hatua zozote za kuboreshwa uhusiano wa Ulaya na Russia, kwa sababu kuishughulisha Russia na vita na mapigano ya muda mrefu ni kwa maslahi ya kistratejia ya Marekani, huku Ulaya nayo ikiwa imebanwa kwenye muungano wa NATO unaoongozwa na Washington.

Mbunge huyo wa bunge la Ulaya ameashiria kuwa, kihistoria, Saudi Arabia ina uhusiano wa karibu na Marekani na ni chaguo mojawapo la kutumiwa kwa ajili ya soko la mafuta; na akabainisha kwamba, Saudia imekataa kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mafuta kwa ajili ya kukabiliana na mgogoro wa nishati uliojitokeza, ambayo ni hatua ya wazi ya kuirubuni Marekani; na matokeo yake ni kwamba, Washington imelegeza kamba kuhusiana na ahadi zake zote za kisiasa za ukiukaji wa haki za binadamu na jinai za kivita zilizofanywa na Saudi Arabia.../