Jun 24, 2022 01:17 UTC
  • Taliban yaitaka Marekani iachie fedha za Afghanistan baada ya tetemeko la ardhi lililoua 950

Kufuatia tetemeko la ardhi lililoua mamia ya watu nchini Afghanistan, serikali ya Taliban nchini humo imeitaka Marekani iachie mabilioni ya dola za Waafghani inazozuilia.

Msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid ametoa mwito huo katika mahojiano na Televisheni ya Sahar ya Iran na kusisitiza kuwa, Marekani inapaswa kuachia haraka iwezekanavyo mabilioni ya fedha za Waafghani inazozuilia.

Ameongeza kuwa, mashirika ya kimataifa, Hilali Nyekundu, na nchi nyingi duniani zikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Pakistan na Russia zimetangaza utayarifu wa kuwasaidia wananchi wa Afghanistan katika kipindi hiki kigumu cha baada ya mtetemeko mkubwa wa ardhi.

Karibu watu 1,000 wameaga dunia na mamia kujeruhiwa katika tetemeko hilo la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 6.1 kwa kipimo cha Rishta, lililoikumba mikoa miwili kusini mashariki mwa Afghanistan juzi Jumatano.

Taathira za zilzala kubwa iliyotikisa Afghanistan

Februari mwaka huu, Ikulu ya White House ilitangaza kuwa utawala wa Joe Biden unapanga kuchukua kwa mabavu nusu ya dola bilioni saba fedha za Afghanistan zinazoshikiliwa katika benki za Marekani na kuzigawa kwa familia za walioathirika na mashambulizi ya Septamba 11 mwaka 2001.

Mara kadhaa nyuma wananchi wa Afghanistan wamefanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul, kulalamikia  hatua hiyo ya Marekani ya kupora mabilioni ya dola za nchi hiyo inayosumbuliwa na mgogoro wa kiusalama na kiuchumi.

Serikali ya Taliban nchini Afghansitan inasisitiza kuwa, kuporwa fedha za nchi hiyo ni wizi wa wazi na dalili ya kuporomoka maadili ya Marekani, huku ikitishia kuangalia upya misimamo na sera za Afghanistan kwa Marekani.

Tags