Jun 24, 2022 07:22 UTC
  • Licha ya kukithiri mauaji, mahakama kuu Marekani yaruhusu ubebaji silaha katika maeneo ya umma

Mahakama Kuu ya Marekani imetoa hukumu ya kuwapa uhuru raia wa nchi hiyo wa kuendelea kutembea na silaha moto katika maeneo ya umma licha ya kukithiri ukatili na mauaji yanayosababishwa na matukio ya ufyatuaji risasi nchini humo.

Marekani imegubikwa na wingu zito la matukio ya ukatili, utekaji nyara watu na mashambulio ya utumiaji silaha. Maelfu ya watu wanauawa na kujeruhiwa kila mwaka katika matukio ya ufyatuaji risasi yanayojiri kwenye maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti rasmi, kwa kila raia 100 wa Marekani kuna silaha moto 120.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, hukumu iliyotolewa na mahakama kuu ya Marekani imebatilisha sheria iliyopitishwa katika jimbo la New York, ambayo iliwataka watu wanaoomba kibali cha kumiliki silaha wathibitishe kuwa wanataka kutumia silaha hizo kwa ajili ya kujilinda.

Sheria ya kubeba silaha ambayo ilipitishwa katika jimbo la New York yapata karne moja iliyopita, ilikuwa imeweka vizuizi kadhaa kwa watu wanaotaka kubeba silaha kwa siri nje ya nyumba zao, lakini hukumu iliyotolewa jana na mahakama kuu ya nchi hiyo imeondoa vizuizi hivyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa mahakama kuu ya Marekani kuitambua kuwa ni haki ya wananchi kubeba silaha katika maeneo ya umma. Hukumu hiyo ni ushindi kwa wanaounga mkono watu kutembea na silaha katika nchi hiyo ambayo inashuhudia mpasuko mkubwa wa mitazamo kuhusu namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili na mauaji yanayosababishwa na utumiaji wa silaha moto.../