Jun 24, 2022 10:52 UTC
  • Jamii ya Kimataifa yatakiwa kutoa msaada zaidi kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi Afghanistan

Afghanistan inahitaji msaada wa kimataifa zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote mwingine.

Tetemeko la ardhi lililotokea katika jimbo la Khost nchini Afghanistan na kusababisha hasara kubwa ya mali na nafsi, limezidisha udharura wa kutumwa misaada ya dharura kwa Waafghani. Hata hivyo, hadi tunaandika uchambuzi huu ni nchi tatu tu, Iran, Qatar na Pakistan, ambazo zilikuwa zimetuma msaada kwa watu wa Afghanistan.

Karibu watu 1,000 wameaga dunia na mamia kujeruhiwa katika tetemeko la ardhi lililoikumba mikoa miwili kusini mashariki mwa Afghanistan, Jumatano iliyopita.

Kwa kuzingatia misimamo makhususi ya nchi za Magharibi hususan Marekani kuhusu Afghanistan, hakutarajiwi misaada ya maana ya nchi hizo kwa watu wa Afghanistan, lakini Waafghani wanataraji kwamba Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kama jumuiya ya nchi za Kiislamu, itakusanya, kupokea na kutuma misaada ya kifedha ili kuokoa watu waliodhulumiwa kwa miaka mingi wa Afghanistan, haraka iwezekanavyo. 

Shehena ya kwanza ya misaada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi, Afghanistan.

Soroush Amiri, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan amesema: "Wakati nchi za Magharibi zimeisahau Afghanistan kwa sababu za kisiasa na hazijali wala kutilia maanani hali ya watu wa nchi hiyo, nchi za Kiislamu zina majukumu mazito ya kuwasaidia watu wa Afghanistan na hazipaswi kutosheka kwa kutoa tamko tu." Watu wa Afghanistan wanakabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi na kimaisha, na kwa wakati huu wanasumbuliwa sana na uhaba wa vifaa na zana za kuondoa vifusi na kuokoa watu walionasa katika nyumba zilizoharibiwa na tetemeko la ardhi la hivi majuzi. Kwa msingi huo, kufumbia macho mateso ya watu wa Afghanistan ni uhalifu usiosameheka. Kwa sababu masuala ya kibinadamu katika nchi hiyo hayapaswi kufungamanishwa na masuala ya kisiasa, huku mamilioni ya watu wasio na hatia wakiachwa peke yao bila ya msaada wowote.

Msimamo wa Marekani na washirika wake wa Kimagharibi wa kupuuza maafa yanayowapata watu wa Afghanistan ni ishara ya kutowajibika kwa nchi hizo na doa la aibu na fedheha katika kipaji cha nchi hizo zinazodai na kujigamba kwamba ndio watetezi wakuu wa haki za binadamu! 

Ali Wahidi, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan anasema: "Marekani haijawahi kusimama pamoja na watu wa Afghanistan na imekuwa ikiwatazama kwa mujibu wa sera zake za kikoloni; na  kwa kupora na kuzuilia fedha za watu wa Afghanistan, imeonyesha kuwa hali yao mbaya haina umuhimu wowote kwa serikali ya Washington."

Alaa kulli hal, watu wa Afghanistan ambao wako katika hali mbaya zaidi, hasa baada ya tetemeko la ardhi hivi karibuni, wanahitaji msaada zaidi kuliko hapo awali. Wakati huo huo, Waafghani wana matarajio makubwa zaidi kwa nchi za Waislamu kuliko nchi nyingine. 

Wafanyakazi wa Hilali Nyekundu ya Iran wakitoa misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi nchini Afghanistan.

Mbali na hayo, wananchi wa Afghanistan wanatarajia kuona nchi jirani na na zile zinazotafuta manufaa ya kiuchumi nchini Afghanistan, zikiingia katika medani na kuchukua hatua za kivitendo za kutoa msaada wa dharura kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi badala ya kuketi kando na kukosoana wao kwa wao. Kwa sababu katika mazingira ya sasa watu wa Afghanistan hawahitaji huruma na maneno matupu, na hapana shaka kuwa vitendo na hatua zitakazochukuliwa na nchi mbalimbali ndizo zitakazowaonesha nani rafiki na nani adui wa taifa hilo.