Jun 25, 2022 03:04 UTC
  • Wananchi wa Korea Kusini waandamana kupinga ngao ya Marekani ya THAAD

Kwa mara nyingine wananchi wa Korea Kusini wamefanya maandamano kupinga mpango wa kusimikwa ngao ya makombora ya kisasa ya Marekani aina ya THAAD ndani ya nchi yao.

Malefu ya Wakorea Kusini jana Alkhamisi waliandamana na kukusanyika karibu na Ofisi ya Rais katika wilaya ya Yongsan, katikati ya mji mkuu wa nchi hiyo, Seoul, huku wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe za kupinga kuwekwa ngao hiyo ya Marekani nchini kwao.

Viongozi wa maandamano hayo wameviambia vyombo vya habari mjini Seoul kuwa, mchakato wa kusimikwa ngao ya makombora ya Marekani ya THAAD unafanyika kinyume cha sheria, kwa kuwa unafanyika bila ridhaa ya Bunge na wananchi wa nchi hiyo.

Duru mpya ya maandamano ya wananchi wa Korea Kusini katika kupinga ngao ya makombora ya Marekani ya THAAD imeanza baada ya Rais Yoon Suk-yeol aliyeingia madarakani Mei 10 kutoa amri ya kuharakishwa shughuli za uwekaji ngao hiyo ya Marekani nchini humo.

Waandamanaji Korea Kusini

Katika miezi ya hivi karibuni, polisi ya Korea imekuwa ikipeleka vifaa na suhula za kufungwa ngao ya THAAD katika eneo husika mara mbili hadi tatu kwa wiki, lakini kuanzia Juni 7, upelekaji wa vifaa hivyo umeongezeka hadi mara tano kwa wiki.

Wananchi wa Korea Kusini wanapinga uwekaji wa ngao hiyo ya Marekani kutokana na sababu kadhaa; kubwa zaidi ikiwa ni taathira hasi kwa mazingira na afya zao, na pia kuhatarisha usalama wao.

Tags