Jun 25, 2022 03:07 UTC
  • Uchina yaonya juu ya upanuzi

Huku kukiwa na msuguano unaozidi kukua, China imeutaka muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi (NATO) kujiepusha na jaribio la kuanzisha Vita Baridi vipya, ikieleza jitihada zake za kujipanua zaidi katika eneo la Asia na Pasifiki kuwa hatari.

Tahadhari hiyo imetolewa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Wang Wenbin ambaye amewashutumu viongozi wa shirika la NATO kuwa wanatoa matamshi ya uchochezi na kusema kuwa, muungano huo unaoongozwa na Marekani ni zao la kipindi cha Vita Baridi.

"Tunatoa wito kwa NATO kukoma kueneza ripoti za uongo au kutoa kauli za kichochezi dhidi ya China, na kuacha jitihada za kuanzisha vita baridi vipya," Wang amewaambia waandishi wa habari.

Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg Jumatano iliyopita alisema kwamba, kwa vile mkutano wa kilele wa shirika hilo huko Madrid utajadili kadhia ya China katika dhana mpya ya kimkakati, anawakaribisha viongozi wa nchi washirika - Australia, Japan, New Zealand na Korea Kusini - kwenye mkutano huo.

Stoltenberg ametoa wito kwa wanachama wa NATO "kutilia maanani kasi ya kukua na kustawi kwa China", akiongeza kuwa anatarajia kwamba, washirika watatangaza kuwa China inatoa changamoto kwa maadili, maslahi na usalama wao."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amekosoa matamshi ya Stoltenberg na kuutaja muungano wa kijeshi wa NATO kuwa ni "chombo ambacho Marekani inakitumia kudumisha ubeberu wake".