Jun 25, 2022 11:38 UTC
  • Wamarekani waghadhibishwa na marufuku ya uavyaji mimba nchini humo

Maandamano makubwa yameshuhudiwa katika miji na majimbo mbalimbali ya Marekani, kulalamikia hatua ya Mahakama ya Juu ya nchi hiyo ya kutengua haki ya kuavya mimba.

Maelfu ya Wamarekani walioshiriki maandamano ya jana walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe za kupinga hukumu hiyo, baadhi yakiwa yameandikwa "Mwili wangu, Chaguo langu."

Katika hukumu ya jana Ijumaa, Mahakama ya Juu ya Marekani ilibatilisha hukumu iliyotolewa mwaka 1973 katika kesi mashuhuri ya 'Roe dhidi ya Wade' iliyosema kuwa wanawake nchini humo wana haki ya kikatiba ya kuavya mimba.

Uamuzi wa jana unaonekana kuwa ushindi mkubwa kwa wafuasi wa chama cha Republican, ambao wamekuwa wakijinadi kuwa watetezi wa uhai nchini humo, na kusisitiza juu ya haki ya kijusi kuendelea kuwa na uhai kwenye tumbo la mama yake na kutaka uavyaji mimba udhibitiwe zaidi.

Hii ni katika hali ambayo kundi jingine linalojiita watetezi wa haki ya kuchagua, linadai kuwa mama mjamzito ana haki ya kuchagua kati ya kuavya au kuendelea kubeba mimba hadi atakapojifungua.

Rais Biden wa Marekani

Rais Joe Biden wa Marekani ni miongoni mwa shakhsia wa Marekani walioukosoa uamuzi wa jana wa Mahakama ya Juu ya nchi hiyo, akidai kuwa hukumu hiyo imeirejesha Marekani miaka 150 nyuma.

Biden amesema: Wanawake wa nchi hii wana mamlaka ya kuamua mustakabali wanaoutaka. Afya na uhai wa wanawake wa nchi hii sasa upo hatarini.

Tags