Jun 25, 2022 11:41 UTC
  • Russia: Hatutajiunga na Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema Moscow haitajiunga na Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia (TPNW).

Maria Zakharova amesema Russia kama mataifa mengine yanayomiliki silaha za nyuklia haikushiriki kongamano la kwanza la nchi-washiriki wa mkataba huo, kwa kuwa mkutano huo haukutilia maanani hali halisi ya kisiasa, kijeshi na kujiopolitiki katika kona mbalimbali za dunia hii leo.

Amesema kupigiwa upatu Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia (TPNW) kutazidisha mifarakano baina ya mataifa, na kunadhalilisha uwepo wa Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Nyuklia NPT.

Zakharova ameeleza bayana kuwa, "Hatuoni njia zozote halisi za kutekeleza, au hatua za kivitendo za kupunguza moja kwa moja silaha za nyuklia."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesisitiza kuwa, kuasisiwa Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Nyuklia kumeharakishwa, na kwamba hatua hiyo ghalati haitakuwa na tija yoyote.

Kichwa cha silaha ya nyuklia ya Marekani

Kauli ya Russia inakuja siku chache baada ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) kuonya kuwa, akiba ya silaha hatari za nyuklia duniani inatazamiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka michache ijayo.

Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi hiyo, Marekani na Russia zingali zinamiliki zaidi ya asilimia 90 ya silaha hizo za nyuklia duniani. Russia inaongoza kwa kuwa na vichwa vya makombora ya nyuklia 5,977, huku Marekani ikifuatia kwa vichwa 5,428.

Tags