Jun 26, 2022 02:27 UTC
  • China: Kuwepo kijeshi Marekani katika Ghuba ya Taiwan ni tishio kwa amani ya dunia

Afisa mmoja wa jeshi la China amesema, kuruka ndege za kivita na za ugunduzi za Marekani katika anga ya Ghuba ya Taiwan ni kitendo cha kichochezi na tishio kwa amani ya dunia.

Beijing inaitambua Taiwan kuwa sehemu ya ardhi kuu ya China na inazichukulia harakati za kijeshi za Marekani na uuzaji wa silaha zake kwa Taiwan kuwa ni ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala ya China zinazokwenda kinyume pia na sera ya "China moja iliyoungana". Hata hivyo Marekani imetuma manowari yake kwenye langobahari la Taiwan na kuongeza misaada ya kijeshi kwa kisiwa hicho. Hatua hiyo imezidisha mivutano na hali ya wasiwasi katika eneo hilo licha ya indhari za mara kadhaa zilizotolewa na China.

Kwa mujibu wa tovuti ya wizara ya ulinzi ya China, msemaji wa kamandi ya eneo la Mashariki ya jeshi la China Xi Yei ameeleza katika taarifa kwamba, kupaa kwa ndege za kivita na za ugunduzi za Marekani katika anga ya Ghuba ya Taiwan kunavuruga hali ya eneo  na kuhatarisha amani na uthabiti katika ghuba hiyo.

Afisa huyo wa jeshi la China ameongezea kueleza katika taarifa yake: " tunatangaza wazi kwamba tunapinga vikali hatua hii ya Marekani na tunawaweka askari wa jeshi la China katika hali ya juu kabisa ya tahadhari kwa ajili ya kulinda mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi yetu".

Ghuba ya Taiwan imekuwa eneo la mzozo na mvutano tangu mwaka 1949, kwa sababu wakati China inaitambua kuwa ni sehemu ya ardhi yake, Marekani inadai kwamba ghuba hiyo ni njia ya maji ya kimataifa.../

Tags