Jun 26, 2022 07:25 UTC
  • Mji wa Sievierodonetsk watekwa kikamilifu na jeshi la Russia huko Ukraine

Majeshi ya Russia yamechukua udhibiti kamili wa mji wa mashariki mwa Ukraine wa Sievierodonetsk. Mji huo umetekwa baada ya wiki kadhaa za mapigano ya umwagaji damu zaidi katika vita vya sasa nchini Ukraine.

Kutekwa mji wa Sievierodonetsk - ambayo wakati mmoja ilikuwa makazi ya zaidi ya watu laki moja (100,000) - ni ushindi mkubwa zaidi wa Russia tangu kutwaliwa bandari ya Mariupol mwezi uliopita.

Maafisa wa kijeshi katika eneo hilo walisema siku ya Ijumaa kwamba wanajeshi wa mwisho wameamriwa kuondoka kwa sababu haiwezekani tena kuendelea kulinda maeneo yao.

Mji wa Sievierodonetsk ulikuwa moja ya ngome kuu za mwisho za jeshi la Ukraine katika eneo hilo.

Kamanda mkuu wa kijeshi mashariki mwa Ukraine amesema, jeshi liliamua kuondoka katika mji huo kwa sababu idadi ya vifo katika maeneo yasiyo na ulinzi imara inaweza kuongezeka siku baada ya siku.

Sievierodonetsk, Ukraine

Ripoti zinasema jeshi la Russia imewakamata matema makumi ya wanajeshi wa Ukraine katika mji huo.

Russia ilianzisha oparesheni za kijeshi dhidi ya Ukraine mwezi Februari mwaka huu baada ya nchi hiyo kukataa kutekeleza mapatano ya Minsk na pia baada ya maeneo ya Donetsk na Luhansk kujitangazia uhuru ambao ulitambuliwa rasmi na Moscow.

Russia pia inasema oparesheni hiyo inalenga kuwaondoa Wanazi Mamboleo nchini Ukraine na kuizuia nchi hiyo kuwa kambi ya muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi, NATO, ambao umekuwa ukitekeleza stratijia ya kichokozi ya kukaribia mipaka ya Russia.