Jun 26, 2022 08:18 UTC
  • Wimbi la hasira latanda Indonesia dhidi ya klabu ya usiku iliyomvunjia heshima Mtume na Bibi Maryam

Polisi ya Indonesia imetangaza kuwakamata watu 6 wanaofanya kazi katika mtandao wa baa na vilabu vya usiku, kwa tuhuma za kudharau dini, huku kukiwa na wimbi kubwa la hasira dhidi ya klabu hizo baada ya kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) na Bibi Maryam (as).

Umati wa waandamanaji ulikusanyika mbele ya baa katika mji wa Bogor, kusini mwa Jakarta, kufuatia mtandao wa baa na vilabu vya usiku vya "Holywings", kutuma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii ukitangaza kuwa utatoa pombe bure kwa kila mtu anayeitwa Muhammad au Maryam.

Waandamanaji hao wametoa wito wa kuchukuliwa hatua dhidi ya waliohusika na kitendo hicho kwa sababu wamevunjia heshima Uislamu na Ukristo.

Mashirika 4 ya kitaifa ya vijana nchini Indonesia - nchi kubwa zaidi ya Kiislamu kwa idadi ya watu - yamewasilisha malalamiko kwa polisi dhidi ya mtandao wa baa na vilabu hivyo na matawi yake mbalimbali.

Mkuu wa Polisi wa Jakarta Kusini, Budi Hrdi Susianto amesema: "Washukiwa sita wametambuliwa na wote wanafanya kazi katika kampuni hiyo."

Polisi wamesema kwamba waliokamatwa wanakabiliwa na mashtaka kadhaa, ikiwa ni pamoja na kudharau na kueneza chuki za kidini, na kuongeza kuwa wanakabiliwa na kifungo cha jela cha hadi miaka 10 ikiwa watapatikana na hatia ya mashtaka hayo.