Jun 26, 2022 11:17 UTC
  • Marekani yaondoa baadhi ya masharti ya kuwasajili vijana jeshini

Jeshi la Marekani limefuta baadhi ya vigezo na masharti ya kusajili vijana jeshini, huku nchi hiyo ikikabiliwana na mgogoro mkubwa wa vijana wengi kukataa kujiunga na vikosi hivyo vya ulinzi.

Tovuti ya habari ya military.com imeripoti kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Marekani imelazimika kuondoa akthari ya masharti iliyokuwa imeanisha kwa ajili ya kuwasajili vijana jeshini, kutokana na idadi ndogo ya watu wanaojitokeza kujiunga na vikosi hivyo vya ulinzi ya US.

Sasa vijana wanaotaka kujiunga na jeshi la nchi hiyo hawatatakiwa kuwa na kiwango cha juu sana cha elimu, na vile vile wenye michoro ya tatoo mwilini hawatazuiwa tena kujiunga na jeshi hilo, kama ilivyokuwa hapo awali.

Haya yanajiri wakati huu ambapo idadi ya askari wanaokimbia kuhudumu ndani ya jeshi la Marekani ikizidi kuongezeka kila uchao, huku suala la matatizo ya kisaikolojia likitajwa kuwa ndio sababu.

Hivi karibuni, Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilitoa ripoti mpya na kusema kuwa, idadi ya wanajeshi wa Marekani wanaojiua na wakiwa jeshini imeongezeka kwa asilimia 46.

Inaarifiwa kuwa, janga la corona ni miongoni mwa sababu za kuongezeka kesi za kujiua wanajeshi wa Marekani.

Tags