Jun 27, 2022 07:43 UTC
  • Putin kufanya safari ya kwanza nje ya nchi tangu Russia ilipoanzisha vita dhidi ya Ukraine

Vyombo vya habari vya Russia vimetangaza kuwa rais Vladimir Putin wa nchi hiyo atafanya safari ya kwanza nje ya nchi tangu vilipoanza vita nchini Ukraine kwa kutembelea nchi mbili za eneo la Asia ya Kati.

Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari Putin atasafiri wiki hii kuelekea Tajikistan na Turkmanestan.

Ziara ya mwisho kufanywa na rais wa Russia nje ya nchi kabla ya kuanza vita vya Ukraine ilikuwa ni ya kuitembelea China mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu.

Zaidi ya miezi minne imepita tangu vilipoanza vita vya Ukraine, vita ambavyo Russia inasema imevianzisha kwa lengo la kuipokonya silaha Ukraine na kufuatia ombi lililowasilishwa kwa nchi hiyo na viongozi wa maeneo ya Donatsk na Luhansk yaliyoko kwenye eneo la Donbas mashariki ya Ukraine.

Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitiza pia kwamba lengo la operesheni ya kijeshi ya nchi yake ndani ya Ukraine ni kutokomeza pia Unazi.

Kwa upande wao, Marekani na nchi za Magharibi zimekoleza moto wa vita hivyo kwa kuipelekea Ukraine silaha na zana mbalimbali za kivita.

Russia imekuwa ikionya na kutoa indhari kwamba silaha na zana za kijeshi ambazo Mareani na Ulaya zinaipatia Ukraine zinashadidisha mzozo wa kivita wa nchi hiyo na zitakuwa na matokeo hasi yasiyoweza kutabirika.../

 

Tags