Jun 28, 2022 02:46 UTC
  • UN yatahadharisha juu ya uwezekano wa kuongezeka uzalishaji wa mihadarati huko Ukraine

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, vita vinavyoendelea huko Ukraine vinaweza kusababisha ongezeko la uzalishaji haramu wa madawa ya kulevya nchini humo.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayohusika na Jinai Mihadarati (UNODC) imeeleza kuwa, uzoefu uliopo katika maeneo ya Mashariki ya Kati ya Kusini Mashariki mwa Asia unaonyesha kuwa, maeneo yaliyoathiriwa na vita na mizozo yanaweza kutumiwa kama kichocheo cha kuzalisha madawa ya kulevya. UNODC imebainisha haya katika ripoti yake ya kila mwaka.

Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, idadi ya maabara zilizovunjwa za kutengeneza dawa za kulevya aina ya amphetamine nchini Ukraine ziliongezeka kutoka 17 mwaka 2019 na kufikia 79 mwaka juzi wa 2020; na kwamba idadi hiyo ni kubwa zaidi za maabara zilizonaswa zikitengeneza dawa za aina hiyo zilizoripotiwa katika nchi yoyote mwaka juzi wa 2020.  

Uwezo wa sasa wa Ukraine kuzalisha dawa za kulevya za kemikali unaweza kuongezeka pakubwa kutokana na kuendelea vita nchini humo. Wataalamu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayohusika na Jinai na Mihadarati (UNODC) wanasema, katika maeneo yaliyoathiriwa na mizizo hakuna polisi wanaofanya msako na kufuatilia maabara zinazofanya shughuli hiyo. 

Taarifa ya Unodc imeendelea kusema kuwa, hali ya mambo huko Afghanistan, nchi ambayo mwaka jana ilizalisha asilimia 86 ya afyuni ya dunia nzima, itachagiza uzalishaji wa mihadarati  hiyo.

Kilimo cha mihadarati aina ya afyuni (Opium) nchini Afghanistan.

Watu wanaokadiriwa kuwa milioni 284 yaani mtu mmoja kati ya kila watu 18 duniani wenye umri kati ya miaka 15 na 64, walitumia afyuni mwaka uliopita wa 2021.

Tags