Jun 28, 2022 07:55 UTC
  • Maiti 46 zapatikana ndani ya lori jimboni Texas, Marekani

Miili 46 imepatikana ndani ya lori lililokuwa limeegeshwa karibu na kambi ya kijeshi ya Lackland jijini San Antonio, katika jimbo la Texas nchini Marekani.

Duru za habari zinaarifu kuwa, maiti hizo zilipatikana jana Jumatatu ndani ya lori lililokuwa limetelekezwa katika eneo lisilo na shughuli nyingi kusini magharibi mwa jiji la San Antonio, karibu na makutano ya barabara ya Cassin Drive na Quintana.

Polisi katika jimbo la Texas imesema wakati maiti hizo zilipopatikana jana Jumatatu, kiwango cha joto katika maeneo ya kusini mwa jimbi hilo ilikuwa nyuzijoto 39.4.

Afisa wa polisi ambaye amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu amesema nusu ya watu waliokuwa ndani ya lori hilo wameaga dunia, na kwamba wengine 16 wamepelekewa hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Vyombo vya usalama nchini Marekani vimesema yumkini watu waliokuwa kwenye lori hilo ni wahajiri waliongizwa nchini humo kinyume cha sheria.

Mpaka wa Marekani na Mexico ni lango kuu la magendo ya binadamu, lakini msimu huu wa joto kali jimboni Texas unaifanya biashara hiyo haramu iwe hatari zaidi kwa wahajiri.

Tags