Jun 28, 2022 09:56 UTC
  • Gavana wa Texas: Biden ndiye wa kulaumiwa kwa

Gavana wa Texas nchini Marekani amemlaumu Rais Joe Biden wa nchi hiyo kuwa ndiye wa kulaumiwa kwa vifo vya makumi ya wahajiri ambao miili yao imepatikana ikiwa imetelekezwa katika lori kwenye jimbo hilo.

Ni baada ya maafisa wa Texas kukuta maiti za watu wasiopungua 46 ndani ya lori lililokuwa limeegeshwa karibu na kambi ya kijeshi ya Lackland jijini San Antonio, nchini Marekani.

Gavana wa Texas, Greg Abbott amesema siasa za serikali ya Biden kuhusu wahajiri ndizo zinazopaswa kulaumiwa kutokana na vifo hivyo.  

Greg Abbott amesema janga hili linaonesha matokeo mabaya ya hatua ya Biden ya kukataa kutekeleza sheria. 

Maafisa kadhaa wa Marekani, akiwemo Seneta wa Texas, Ted Cruz, wameulaumu utawala wa Biden kwa tukio hilo na kuuita ugunduzi wa miili ya wahamiaji hao kuwa "wa kutisha."

Duru za habari zinaarifu kuwa, maiti hizo zilipatikana jana Jumatatu ndani ya lori lililokuwa limetelekezwa katika eneo lisilo na shughuli nyingi kusini magharibi mwa jiji la San Antonio, karibu na makutano ya barabara ya Cassin Drive na Quintana.

Texas

Afisa wa polisi ambaye amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu amesema nusu ya watu waliokuwa ndani ya lori hilo wameaga dunia, na kwamba wengine 16 wamepelekewa hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Mkuu wa Polisi wa eneo la San Antonio amelitaja tukio hilo kuwa ndilo baya zaidi katika jiji hilo na kuongeza kuwa, hadi sasa watu watatu wamekamatwa kuhusiana na kesi hiyo.

Tags