Jun 28, 2022 13:30 UTC
  • Twitter yaungana na serikali ya India kuwakandamiza Waislamu, yafunga akaunti za watetezi wao

Waandishi wa habari na wanaharakati wamepinga ongezeko la hatua za serikali ya India ikishirikiana na mtandao wa kijamii wa Twitter za kuwabana watu mashuhuri wanaowatetea Waislamu na kuunga mkono harakati za maandamano yanayopinga ukandamiza wa serikali ya New Delhi dhidi ya wafuasi wa dini hiyo.

Kampeni hii ya kuwakandamiza watetezi na wanaharakati wanaowatetea Waislamu imevuka mipaka ya mtandao na sasa baadhi ya wanaharakati hao wanatiwa nguvuni.

Mtandao wa mashirika ya vyombo vya habari vya kidijitali umetangaza kuwa, polisi wa Delhi wamemkamata mwandishi wa habari Muislamu, Mohammed Zubair, ambaye alishiriki katika kuanzisha tovuti ya kufuatilia ukweli, na kumtuhumu kwamba amevunjia heshima itikadi za kidini kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter.

Mtandao huo umelaani kukamatwa kwa mwanahabari huyo Muislamu, ukieleza kuwa ni jaribio la kumuwekea vikwazo kwa sababu ya kazi yake ya uandishi wa habari. Mtandao huo umeeleza kuwa Zubair - ambaye mara kwa mara hutumia Twitter kuzungumzia mateso ya Waislamu walio wachache nchini India - alikamatwa chini ya vifungu viwili vya Sheria ya Kuhifadhi Maelewano ya Kidini.

Saa chache kabla ya kukamatwa kwake, Zubair alisema katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kwamba amepokea barua pepe kutoka kwa uongozi wa Twitter ikimuarifu kwamba tovuti hiyo imefuta ujumbe wake uliokuwa na video ya mwanaharakati wa mrengo wa kulia wa Kihindu akitaka Waislamu washambuliwe na mali zao ziporwe.

Hapo awali, mamlaka za India zilimkamata Testa Sittalvad, mwanaharakati mashuhuri anayejulikana kwa kuwatetea wahanga wa Kiislamu wa mauaji ya Gujarat ya 2002.

Wakati huo huo Rana Ayyub, mwandishi wa habari mashuhuri wa Kiislamu anayelengwa kwa kampeni na hujuma za mrengo wa kulia za Kihindu, amesambaza baruapepe kutoka taasisi ya Twitter ikisema kwamba akaunti yake imepigwa marufuku nchini India.

Mwezi uliopita wa Juni Taasisi ya haki za binadamu ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ililaani vitendo vya kibaguzi dhidi ya Waislamu nchini India.

Polisi wa India wakiwakandamiza Waislamu.

Taasisi hiyo ilitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuiwajibisha India kwa ukiukaji wa haki za binadamu za walio wachache na kukomesha uhasama wake.

Tags