Jun 29, 2022 02:18 UTC
  • Juhudi za G7 za kukabiliana kiuchumi na China

Viongozi wa mataifa saba yaliyoendelea kiviwanda, G7, wameafiki kuzindua mpango kabambe wa kuwekeza katika miundo msingi kwenye nchi zinazoendelea. Viongozi hao wametangaza kuwa, nchi za G7 zinakusudia kutenga dola bilioni 600 kwa ajili ya mpango huo ifikapo 2027.

Akitangaza kwamba Washington imeahidi kutoa dola bilioni 200 kwa ajili ya bajeti hiyo, Rais wa Marekani Joe Biden amesema: "Huu si msaada au hisani, bali ni uwekezaji, na matunda yake yatakuwa ya pande zote."

Mpango huo ambao umewasilishwa kwa anwani ya "Ushirikiano kwa ajili ya Miundombinu na Uwekezaji wa Kimataifa", kwa hakika ni jina jipya la mpango ulioidhinishwa katika mkutano wa kilele wa G7 wa mwaka jana nchini Uingereza iliopewa jina la "Ujenzi wa Dunia Bora".

Chini ya mpango huo mpya, katika kipindi cha miaka mitano ijayo jumla ya dola bilioni 600 zitatumika katika miradi kama vile kujenga kituo cha kuzalisha umeme wa jua nchini Angola, kupanua nyaya za mawasiliano chini ya maji kwa ajili ya kujenga mtandao wa intaneti wenye kasi kubwa, kujenga hospitali na kuzalisha chanjo nchini Senegal na Ivory Coast, na kusaidia mfuko wa kimataifa wa huduma kwa watoto.

Mpango huo unakuja wakati mwaka 2021 China iliwekeza zaidi ya dola bilioni 59 katika mradi wa The Belt and Road Initiative (BRI) ili kuunda soko kubwa la pamoja na kujenga miundombinu katika nchi zinazoendelea. Mpango huo wa BRI ambao awali ulilenga nchi zilizo karibu na Njia ya kihistoria ya Hariri na nchi za Kusini na Kusini Mashariki mwa Asia, sasa umepanuka na kujumuisha miradi mingine barani Afrika na Amerika Kusini. 

Dakta Arash Raeisinejad anaandika kuhusiana na suala hili kwamba: "Juhudi za Beijing za kuzindua na kuendeleza Njia mpya ya Hariri zinaweza kuonekana kuwa ni mashindano ya kidhahiri ya kiuchumi baina ya Beijing-Washington; lakini kwa undani na kwa kina, Njia mpya ya Hariri ni mpambano wa jiografia ya kisiasa kati ya Uchina na Merekani kwa ajili ya kuidhibiti dunia katika karne ya 21."

Nchi za Magharibi sasa zinatangaza bajeti ya dola bilioni 600 ilhali sio tu kwamba vyanzo vya fedha hizo havijulikani, lakini pia nchi hizo zenyewe zinakabiliwa na migogoro mikubwa ya kiuchumi na nakisi ya bajeti. Kwa sasa nchi nyingi za Ulaya zinakabiliwa na malalamiko ya kijamii, ukosefu wa ajira na mfumuko wa bei. Katika upande mwingine Marekani nayo iko katika hali mbaya ya kiuchumi, kwa kadiri kwamba Mkurugenzi Mkuu wa IMF, Kristalina Georgieva ameonya kwamba, huenda Marekani ikalazimika kustahamili "maumivu makali" ili kukabiliana na mfumuko wa bei unaoendelea kuongezeka. 

Itakumbukwa kuwa, mwaka jana serikali ya Joe Biden ilipendekeza bajeti ya takriban dola trilioni nne kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu nchini Marekani, lakini Kongresi hatimaye ilikubali kutenga dola trilioni moja tu kujenga upya miundombinu iliyochakaa ya nchi hiyo. Wakati huo huo hivi majuzi Seneta Bernie Sanders alionya kwamba miundombinu ya Marekani imo katika hali ya kusambaratika. Vilevile Chama cha Wahandisi wa Ujenzi cha Marekani kimesema katika ripoti yake kwamba nchi hiyo inasumbuliwa na upungufu wa dola trilioni 2 na bilioni 590 kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya miundombinu; suala ambalo linalazimu kuzidishwa matumizi ya serikali kwenye kukarabati madaraja, barabara zilizochakaa na mambo mengine.

Joe Biden

Kwa mazingira haya inaonekana kuwa, uamuzi wa kutekeleza mpango eti wa "Ujenzi wa Dunia Bora" wa nchi za G7 unakabiliwa na matatizo makubwa, hasa katika kipindi cha sasa ambapo vita vya Ukraine vimezidisha mashinikizo ya kiuchumi kwa nchi za Magharibi, na hatua yoyote ya uchochezi dhidi ya China inaweza kuilekeza na kuikurubisha zaidi Beijing kwa Moscow.

Tags