Jun 29, 2022 03:42 UTC
  • Marais wa Iran na Russia wanakutana leo Ashgabat

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo anakutanza na mwenzake wa Russia Vladimir Putin katika kikao kitakachofanyika katika mji mkuu wa Turkmenistan, Ashgabat.

Kwa mujibu wa taarifa mshauri wa rais wa Russia katika sera za kigeni Yuri Viktorovich Ushakov amesema Rais Putin leo atashiriki katika kikao cha viongozi wa Nchi za Pwani ya Bahari ya Kaspi ambacho kinafanyika mjini Ashgabat nchini Turkmenistan na akiwa hapo atakutana na marais Ebrahim Raisi wa Iran na Ilham Aliyev wa Jamhuri ya Azerbaijan.

Rais Raisi leo Jumatano ameelekea Turkmenistan akiwa anaongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi kushiriki katika Kikao cha Sita cha Viongozi wa Nchi za Pwani ya Bahari ya Kaspi.

Mbali na kuhutubu katika kikao hicho,  rais wa Iran atafanya mazungumzo na marais wengine wanaoshiriki katika kikao hicho.

Baraza la Mawaziri wa Nchi za Pwani ya Bahari ya Kaspi lilikutana jana mjini Ashgabat kujadili ajenda ya kikao cha viongozi leo na kati ya masuala muhimu yaliyojadiliwa ni namna ya kuimarisha ushirikiano wa nchi zinazotumia Bahari ya Kaspi. Viongozi wanaokutana leo wanatazamiwa kuidhinisha mapatano yaliyotayarishwa na baraza hilo la mawaziri.

Nchi za Pwani ya Bahari ya Kaspi ni pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Turkmenistan, Kazakhstan, Russia na Jamhuri ya Azerbaijan.

Bahari ya Kaspi ni ziwa kubwa kabisa duniani lenye eneo la kilomita mraba 371,000 na mjao wa kilomita mraba 78,200 na kimo chake kinafikia mita 1,025.

Huitwa "bahari" kwa sababu maji yake ni ya chumvi ingawa si kali sana kama ya bahari zingine.