Jun 30, 2022 07:45 UTC
  • Kundi la 'Proud Boys' la US lawekwa katika orodha ya magaidi New Zealand

New Zealand imeliweka katika orodha yake ya makundi ya kigaidi kundi la mrengo wa kulia lenye misimamo ya kuchupa mipaka la "Proud Boys" la Marekani.

Baada ya kundi hilo kuorodheshwa katika faharasa ya New Zeland ya makundi ya kigaidi, pamoja na makundi mengine 18 ya kigaidi yakiwemo ya al Qaida na ISIS (Daesh), sasa ni marufuku kulifadhili, kujiunga nalo au kushiriki shughuli zake nchini humo.

Nchi hiyo ya Pacific Kusini ilianza kuchukua hatua za kukabiliana na makundi ya Wazungu wenye misimamo ya kufurutu ada na kujiona bora, kufuatia mauaji ya makumi ya watu misikitini mwaka 2019.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Novemba mwaka 2020, Mahakama Kuu ya New Zealand ilitoa adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa Brenton Tarrant, mzungu gaidi aliyeungama kuwa na imani ya kujiona bora, ambaye aliwaua kwa kuwapiga risasi Waislamu 51 waliokuwa wakisali katika msikiti miwili ya mji wa Christchurch mnamo Machi 15, 2019.

Kongresi ya US ilipovamiwa na genge la kigaidi la 'Proud Boys'

Februari mwaka jana pia, kundi hilo la 'Proud Boys' liliwekwa na Canada katika orodha yake ya makundi ya kigaidi pamoja na makundi ya al Qaida na Daesh (ISIS).

Kundi hilo lilishiriki pakubwa katika uvamizi dhidi ya Kongresi ya Marekani Januari 6 mwaka jana. Tangu mwaka 2016 hadi sasa, kundi hilo la wafuasi wa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump limehusika katika machafuko mbalimbali ya kisiasa nchini humo. 

Tags