Jun 30, 2022 09:22 UTC
  • Kuanza kikao cha sita cha viongozi wa Bahari ya Kaspi huko Ashgabat

Baada ya kusimamishwa kwa mwaka mmoja, kikao cha sita cha viongozi wa nchi tano zinazopakana na Bahari ya Kaspi kilianza Jumatano alasiri huko Ashgabat, mji mkuu wa Turkmenistan.

Awali, kikao hicho kilikuwa kimepangwa kufanyika mjini Ashgabat mwaka jana lakini hofu ya kuenea virusi hatari vya corona na kuwepo kwa vikwazo katika baadhi ya nchi za eneo kulisababisha kuakhirishwa kikao hicho cha kilele hadi mwaka huu wa 2022.

Kikao cha kwanza cha Bahari ya Kaspi   kilifanyika mjini Ashgabat mnamo Mei 2002 kufuatia pendekezo lililotolewa na rais wa wakati huo wa Turkmenistan Safarmurad Niyazov, kwa lengo la kuainisha sheria mpya za uendeshaji mambo katika Bahari ya Kaspi na kwa ushiriki wa marais wa nchi tano. Duru ya pili ya kikao hicho ilifanyika Novemba 2007 mjini Tehran.

Ni wazi kuwa kati ya nchi tano zinazopakana na  Bahari ya Kaspi ambazo ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, Kazakhstan, Turkmenistan na  Azerbaijan, Iran ndiyo nchi inayohesabiwa kuwa njia muhimu zaidi kwa ajili ya Russia na nchi nyingine za Asia ya Kati na Kusini mwa Kaukashia kuweza kufikia maji ya kimataifa.

Marais Ebrahim Raisi wa Iran (kushoto) akiwa na mwezake Vladimir Putin wa Russia pambizoni mwa kikao cha Ashgabat

Iran imeshiriki katika kikao cha kilele cha Ashgabat kwa kiwango cha juu zaidi kiserikali. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Seyyed Ebrahim Raisi, aliwasili nchini Turkmenistan Jumatano, Juni 29 akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa maafisa wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni  wa Iran kwa ajili ya kushiriki katika kikao hicho. Kuwepo ujumbe wa ngazi za juu unaoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kunaashiria kuwa, ujumbe huo wa Iran unakusudia kusaini mikataba muhimu na wawakilishi wengine wa nchi za Kaspi pambizoni mwa kikao cha Ashgabat.

Kuhusiana na hilo, gazeti rasmi la serikali ya Ashgabat, "Turkmenistan Today", limeandika ripoti juu ya mkutano wa kilele wa Kaspi kwa kusema:

Mkutano wa Sita wa mataifa ya Kaspi ikiwa imepita miaka 20 tangu kuasisiwa kwake, utakuwa hatua muhimu kuelekea uwanja wa kufanyika mazungumzo chanya ya kujenga uhusiano kati ya mataifa yanayopakana na Kaspi, ambayo kwa kawaida yana mafungamano ya jadi na ya kirafiki, maelewano na ushirikiano wa kuaminiana.

Awali, mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Kaspi ulikuwa umefanyika katika mji huo huo wa Ashgabat. Mikutano ya baraza hilo ambayo inachukuliwa kuwa utangulizi wa kikao cha viongozi na ambayo maazimio yake hujadiliwa kwenye kikao hicho, mnamo Juni 28 ulijadili na kuafikiana juu ya masuala muhimu ya biashara na usafirishaji na ushirikiano wa pande zote katika nyanja za nishati na masuala yanayohusiana na mazingira.

Hapana shaka kwamba uhifadhi wa mazingira na mfumo wa ikolojia wa Bahari ya Kaspi ni muhimu sana kwa serikali na mataifa yanayoizunguka.

Wakati huo huo, inasemekana kuwa hifadhi nyingi za mafuta na gesi za nchi mbili za eneo ambazo ni Kazakhstan na Azabajani, ziko ndani ya maji ya Bahari ya Kaspi. Nchi hizo mbili hazina mafuta mengi na gesi ya kuchimbwa kwenye nchi kavu, na kwa hivyo zinalazimika kuchimba mafuta na gesi kwenye maji hayo ili kukidhi mahitaji yao ya kifedha.

Sehemu ya ujumbe wa Iran kwenye kikao hicho

Kwa kuzingatia hilo kikao cha kilele cha Ashgabat ni fursa nzuri kwa viongozi wa nchi zinazopaka na Bahari ya Kaspi kujadili na kutia saini mikataba mipya muhimu kuhusu uhifadhi wa mazingira. Hii ni kwa sababu makubaliano yaliyofikiwa huko nyuma kuhusu masuala ya mazingira katika Bahari ya Kaspi yamekuwa yakipuuzwa na baadhi ya serikali za pwani ya bahari hiyo na, hasa Jamhuri ya Azerbaijan na Kazakhstan.

Tafiti zinaonyesha kwamba Bahari ya Kaspi ina hifadhi nyingi za aina za samaki, ikiwa ni pamoja na aina 130 za wanyama. Kwa kuongezea, 90% ya mahitaji ya jamii ya kimataifa kutokana na mayai ya samaki ya caviar yanapatikana kutoka Bahari ya Kaspi. Thamani ya hifadhi hizi inakadiriwa kuwa dola bilioni 500 kwa mwaka.

Jambo la kuzingatia katika suala hili ni ukweli kwamba akiba ya mafuta na gesi asilia huisha baada ya miaka 30 au 50 hivi. Lakini akiba ya samaki inaweza kutumika kwa maelfu ya miaka ikiwa kanuni za mazingira zitazingatiwa na aina za wanyama kulindwa.

Hii ndiyo sababu wanamazingira wengi wanaona kuwa kutiwa saini mikataba ya kulinda mazingira katika Bahari ya Kaspi ni muhimu zaidi kuliko kutiwa saini na nchi za kigeni mikataba yenye thamani ndogo za kifedha na ambayo hufanya uharibifu mkubwa wa kimazingira ikiwa ni pamoja na kuua mamilioni ya wanyama na mimea adimu katika Bahari ya Kaspi.

Tags