Jun 30, 2022 13:31 UTC
  • Kisiwa cha Nyoka
    Kisiwa cha Nyoka

Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kuwa Moscow imeondoa vikosi vyake vyote kwenye Kisiwa cha Nyoka cha Ukraine kwenye Bahari Nyeusi ili kuonyesha nia njema.

Taarifa ilitotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kwamba, leo tarehe 30 Juni, vikosi vya jeshi la Shirikisho la Russia, kwa nia njema, vimekamilisha majukumu yao kwenye Kisiwa cha Nyoka na kuondoa kwenye kambi za eneo hilo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Moscow imeionyesha jamii ya kimataifa kwamba Shirikisho la Russia halitatizi juhudi za Umoja wa Mataifa za kuandaa njia ya kibinadamu kwa ajili ya usafirishaji wa bidhaa za kilimo kutoka Ukraine." 

Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema: "Sasa ni juu ya Kiev kukomesha mzingiro wake katika eneo hilo, kwani Ukraine bado haijaondoa mabomu ya kutega ardhini ambayo yanazuia meli kuondoka kwenye bandari za Bahari Nyeusi."

Kisiwa cha Zmiinyi, kinachojulikana kama Kisiwa cha Nyoka, kiko kaskazini-magharibi mwa Bahari Nyeusi, kilomita 40 kutoka Romania, ambayo kwa sasa ni mwanachama wa NATO. Baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti, kisiwa hicho kilikuwa sehemu ya Ukraine, lakini Bucharest inadai kuwa ni milki yake.

Katika miezi ya hivi karibuni, vikosi vya jeshi la Ukraine vimejaribu kukichukua tena kisiwa hicho kutoka kwenye udhibiti wa Russia, lakini vimeshindwa na kupoteza ndege za kivita, ndege zisizo na rubani na idadi kubwa ya wanajeshi.