Jun 30, 2022 13:35 UTC
  • China yaitaka Marekani kurekebisha makosa yake mkabala wa Iran

China imeitaka Marekani irekebishe makosa yake katika mienendo yake dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya China imesema kuwa Washington, ikiwa ni mwanzilishi wa mgogoro wa nyuklia wa Iran, inapaswa kurekebisha makosa yake na kujibu wasiwasi wa Tehran.

Beijing imekuwa ikiilaumu Marekani mara kwa mara kwa hali ya sasa ya miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran na kuitaka Washington ichukue maamuzi muhimu ya kisiasa haraka iwezekanavyo.

Wakatii huo huo Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan'ani ameashiria mazungumzo yanayojadili suala la kuondolewa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran huko Doha nchini Qatar na kusema: Mazungumzo ya kina yaliendelea mjini Doha siku za Jumanne na Jumatano kwa upatanishi wa Enrique Mora, Naibu Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya (EU).

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesisitiza kuwa: Maoni na mapendekezo ya Iran yalitolewa kuhusu masuala yaliyosalia, na upande wa pili pia uliwasilisha mapendekezo yake.

Mazungumzo ya Doha

Kan'ani ameongeza kuwa: "Kama kawaida, Tehran na mpatanishi wa Umoja wa Ulaya zitawasiliana kuhusiana na jinsi ya kuendeleza mazungumzo na hatua inayofuata ya mazungumzo hayo."

Kiongozi wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA, Ali Bagheri Kani, aliwasili Doha Jumanne iliyopita, siku chache baada ya Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Joseph Borrell kuja hapa Tehran kwa ajili ya kujaribu kutanzua kitendawili cha kukwama mazungumzo ya JCPOA huko Vienna nchini Austria.

Tags