Jul 01, 2022 08:03 UTC
  • China yajibu mapigo kwa hati ya mkakati mpya wa NATO dhidi yake

China imekosoa hati ya mkakati na stratejia mpya ya Muungano wa Kijeshi wa NATO na kueleza kwamba muungano huo ni changamoto ya kimfumo kwa usalama na uthabiti wa dunia.

Viongozi wa nchi wanachama wa NATO walifikia mwafaka kuhusu dhana ya mkakati na stratejia mpya ya muungano huo wa kijeshi katika kikao chao kilichofanyika siku ya Jumatano mjini Madrid, Uhispania. Baada ya makubaliano hayo, kwa mara ya kwanza NATO imeihutubu China kwa kuituhumu kuwa inajaribu kuvuruga nidhamu ya dunia. Russia pia imetajwa kuwa ni tishio la moja kwa moja na muhimu zaidi kwa usalama wa nchi wanachama wa NATO.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Zhao Lijian ametoa jibu kuhusiana na kutangazwa mkakati mpya wa NATO unaohusisha nchi hiyo na kusema kuwa, NATO yenyewe ni changamoto ya kimfumo kwa usalama na uthabiti wa dunia.

Zhao Lijian

Lijiian amebainisha kwamba, kwa uongozi wa Marekani, muungano wa kijeshi wa NATO, ambao unajitaja kama nguvu ya kujihami unasababisha mivutano na vita ulimwengu mzima; na ukweli ni kwamba, unawatesa na kuwataabisha walimwengu.

Halikadhalika, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China ameituhumu NATO kuwa inafuata idiolojia ya enzi za Vita Baridi dhidi ya nchi washindani na kutia chumvi katika kauli zake zisizo na msingi wowote dhidi ya nchi hiyo na akautaka muungano huo wa kijeshi ukomeshe lawama na ukosoaji wa kichochezi inaofanya dhidi ya serikali ya Beijing.../

Tags