Jul 01, 2022 08:45 UTC

Rais wa Russia, Vladimir Putin, amelaani "sera za kupenda makuu" za Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO), ambalo anaamini linalenga kuimarisha "ubeberu" wake kupitia vita vya Ukraine.

Putin ameutaja uungaji mkono wa Ulaya kwa Ukraine kwa ajili ya kuendeleza vita na kupinga mazungumzo kuwa unathibitisha na kusadikisha mtazamo wake, akisema kwamba lengo la Wamagharibi na NATO si kulinda maslahi ya Ukraine na watu wake, bali ni kutetea maslahi yao binafsi. Kwa hakika, NATO, ikiongozwa na Marekani, kwa muda mrefu imekuwa ikitafuta adui wa kigeni ili kuweza kuwakusanya pamoja washirika wake.

Vita vya Russia na Ukraine vilianza kufuatia dhamira ya Ukraine ya kutaka kujiunga na shirika la kijeshi la NATO, na misaada ya nchi za Magharibi kwa nchi hiyo imepelekea kurefushwa vita hivyo na kufunga njia ya mazungumzo ya kumaliza vita hivyo. Kwa maneno mengine ni kuwa, misimamo ya kihasama na ya kivita ya NATO na Marekani dhidi ya Moscow na matakwa yake ya kiusalama, imezidisha makabiliano ya kijeshi baina ya Russia na NATO barani Ulaya.

Katika miaka ya hivi karibuni, Washington na NATO zimekuwa zikisisitiza mara kwa mara kwamba Russia ni tishio kwa Ulaya. Hata hivyo ukweli ni kwamba, katika mfumo wa sera yake na kujipanua zaidi upande wa Mashariki katika miongo miwili iliyopita, NATO imefanya juhudi kubwa kuzipa uwanachama nchi za Ulaya ya Kati na Mashariki na kisha Balkan Magharibi katika shirika hilo la kijeshi; na wakati huo huo inafanya mikakati ya kuziingiza katika jumuiya hiyo nchi majirani wa Russia. Hivyo tunaweza kusema kuwa, moja ya malengo makuu ya NATO inayoongozwa na Marekani ni kudhibiti na kuizingira kikamilifu nchi ya Russia. Miongoni mwa malengo mengine ya NATO ni kupanua zaidi shirika hilo la kijeshi la nchi za Magharibi na kuzipa uanachama nchi zaidi za Ulaya na majirani zao. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Liz Truss anasema: "Sera ya mlango wazi ya NATO ni muhimu, na kuongeza kuwa: "Suala muhimu kwa sasa ​​ni kutilia maanani NATO ya kimataifa, kwa sababu wakati tunahakikisha usalama wa eneo la Ulaya, lazima pia tuwe waangalifu juu ya usalama wa eneo la Indo-Pacific."

NATO, chini ya uongozi wa Marekani, inajaribu kupanua wigo wa ushawishi wake dhidi ya China na Russia. Katika mkondo huo vita vya Ukraine sasa vimefungua njia ya kujitanua kwa NATO, kwani nchi za Ulaya zinazoongozwa na Marekani sasa zinatumia kadhia ya Ukraine kwa ajili ya kutekeleza sera zao za kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kupanua ubeberu wao. Ukweli huu unathibitishwa na matamshi ya maafisa wa zamani wa ujasusi na jeshi Marekani waliokiri kwamba, uwepo wa majasusi wa serikali ya Washington huko Ukraine una maana kuwa Marekani iko katika vita vya niaba dhidi ya Russia.

Ni kwa kuzingatia hayo ndiyo maana Rais Vladimir Putin akaonya kuwa: "NATO ni mabaki ya Vita Baridi, na Moscow inaiona kama chombo cha kutekeleza sera ya Marekani."

Itakumbukwa kuwa katika mkutano wa sasa wa viongozi wa NATO nchini Uhispania, Jens Stoltenberg, mkuu wa muungano huo alisisitiza kuwa: "NATO itaiunga mkono na kuisaidia Ukraine maadamu vita vitaendelea." Viongozi wa shirika hilo pia wametayarisha mazingira ya uwanachama wa Sweden na Finland katika jumuiya hiyo.

Pamoja na hayo inatupasa kusema kuwa, sera hii ya kupanua satua na jumuiya ya NATO itakuwa na madhara kwa nchi za Ulaya. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje za Nje ya China, Zhao Lijian anasema: "Wanachama wa NATO wako katika anga na fikra za 'Vita Baridi'. Wanapaswa kuweka kando sera za 'kujenga uadui" na wasifanye jitihada za kuvuruga hali ya mambo katika maeneo mengine ya dunia baada ya Ulaya."

Inaonekana kwamba sera ya sasa ya Ulaya ni ya mwelekeo wa vita, upanuzi wa NATO duniani, pamoja na kudhibiti na kuingilia masuala ya nchi nyingine, suala ambalo hatimaye litazusha mgogoro na mivutano huko Ulaya na Magharibi kwenyewe.

Tags