Jul 01, 2022 10:34 UTC
  • NATO yaonya kuhusu 'vita kamili' na Russia

Muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi-NATO -umeonya kwamba mzozo wa sasa nchini Ukraine, ambako Russia imekuwa ikiendesha operesheni maalumu ya kijeshi, unaweza kugeuka na kuwa vita visivyozuilika kati ya muungano huo wa kijeshi wa Magharibi na Moscow.

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alitoa tahadhari wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Madrid kufuatia mkutano wa kilele uliowashirikisha wakuu wa nchi na serikali wa muungano huo.

"Tunaishi katika ulimwengu hatari zaidi. Tunaishi katika ulimwengu usiotabirika. Na tunaishi katika ulimwengu ambao kwa kweli tuna vita vikali vinavyoendelea Ulaya, na kuna operesheni kubwa za kijeshi ambazo hatujawahi kuziona  Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia," alisema.

"Hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi na kugeuka kuwa vita kamili kati ya Russia na NATO," alionya.

Alisema NATO tayari imeongeza kwa kiasi kikubwa uwepo wake kwenye upande wake wa mashariki kwa kupeleka zaidi ya wanajeshi 40,000 eneo hilo.

Mkusanyiko huo wa kijeshi, alisema, ulikusudiwa kuonyesha Russia  kuhusu utayari wa NATO kijeshi na kivita.

Ukraine imekuwa chini ya operesheni ya Russia tangu Februari 24 ambapo Moscow inasema operesheni hiyo inalenga "kuondoa hali ya kijeshi" eneo la mashariki mwa Ukraine la Donbas.

Rais Putin wa Russia

Huko nyuma mwaka wa 2014, mikoa ya Donetsk na jirani yake Luhansk-ambazo kwa pamoja zinaunda Donbas-zilijitangaza kuwa jamhuri huru, zikikataa kutambua serikali ya Ukraine inayoungwa mkono na muungano wa kijeshi wa NATO.

Akiamuru operesheni hiyo nchini Ukraine, Rais wa Russia Vladimir Putin alisema oparesheni hiyo inalenga "kutetea watu ambao kwa miaka minane walikuwa wakiteswa na kutendewa mauaji ya halaiki na serikali ya Kiev."

Mkuu wa NATO, wakati huo huo, amesema  muungano huo "utasaidia Ukraine kubadilisha vifaa vya zamani vya kijeshi vya enzi ya Sovieti vya Ukraine hadi vifaa vya kisasa vya NATO."

Mapema mwezi uliopita, Putin alionya kwamba nchi yake inaweza kuanza kupanua wigo wa mashambulizi yake nchini Ukraine ikiwa Magharibi itaimarisha usambazaji wake wa silaha kwa nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa sehemu ya Shirikisho la Sovieti.