Jul 01, 2022 10:43 UTC
  • Ajali za barabarani zinaua watu milioni 1.3 duniani kila mwaka

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa duniani kote ajali za barabarani zinachukua maisha ya watu takriban milioni 1.3 kila mwaka ambao ni sawa na zaidi ya watu wawili kila dakika huku wengine milioni 50 wakijeruhiwa.

Pia takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 90% ya vifo hivyo au vifo 9 kati ya 10 vinatokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati.

Na wengine wanaokufa au kifo 1 kati ya vifo 4 vya ajali hizo za barabarani vinawahusu watembea kwa miguu au waendesha baiskeli.

Takwimu hizo zimetolewa huku Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likiwa limeitisha mkutano wa kujadili ajali za barabarani duniani. Mkutano huo ulianza jana tarehe 30 Juni na unamalizika leo chini ya kaulimbiu "Kuufikia mwaka 2030 kwa ajili ya usalama barabarani; kupata muongo wa utekelezaji na utimizajii".

Akizungumzia umuhimu wa kudumisha usalama barabarani mkurugenszi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema  "Usalama barabarani unaathiri kila mtu. Kila siku tunatoka majumbani mwetu kupitia barabara zinazotupeleka kwenye kazi zetu, shuleni na kukidhi mahitaji yetu muhimu ya kila siku. Hata hivyo mifumo yetu ya usafiri inasalia kuwa hatari sana. Hakuna kifo kinachopaswa kukubalika kwenye barabara zetu. Mustakabali wa usafiri unapaswa kukuza afya na ustawi, kulinda mazingira na kufaidisha wote.” 

Ajali ya barabarani nchini Tanzania

Mkurugenzi huyo wa WHO ameongeza kuwa suala la usalama barabarani "Iitahitaji uongozi wa mabadiliko kutoka ngazi za juu za serikali kuweza kuchukua hatua kuhusu azimio la kisiasa ili kutimiza malengo haya." 

WHO imekaribisha tamko la kisiasa au azimio litakalopitishwa na nchi wanachama wakati wa mkutano huo wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu usalama barabarani duniani. 

Azimio hilo linajitolea kupunguza vifo na majeruhi wa ajali za barabarani kwa asilimia 50% ifikapo 2030, ambayo kwa mujibu wa WHO ni hatua muhimu kwa usalama barabarani na uhamaji endelevu.